1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na Haki

Upelelezi wa wanawake waliouliwa Mombasa

29 Septemba 2016

Mashirika ya kutetea haki Kenya yanasema mkasa ambapo polisi iliwauwa wanawake watatu iliodai walikuwa magaidi umekosa mashiko. Watetezi wanasema wanawake hao hawakuwa hatari kama ambavyo ilielezwa na polisi.

https://p.dw.com/p/2Qk4Q
Polisi wakiwekea mpaka eneo ambapo wanawake watatu waliuawa Mombas
Polisi wakiwekea mpaka eneo ambapo wanawake watatu waliuawa MombasaPicha: picture-alliance/AP Photo

Katika taarifa rasmi ya tukio hilo, polisi walizuia jaribio la kigaidi mnamo tarehe 11 mwezi Septemba wakati wanawake hao ambao wanasema kabla ya hapo waliwahi kuandika barua ya kuliunga mkono kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, IS, waliingia katika kituo cha polisi cha Central wakiwa wamejihami kwa visu, mabomu ya petroli na mikanda ya mabomu.

Inasemekana kuwa polisi waliokuwa wakishika doria, waliwafyatulia risasi huku mmoja wa washukiwa akiteketea vibaya kiasi cha kutojulikana kutokana na kulipuka kwa kifaa alichokuwa nacho.

Lakini makundi mawili tofauti ya kutetea haki za binadamu yanayofanya shughuli zao tofauti yalikusanya taarifa tofauti. Kwa uhakika wanasema kuwa wasichana hao watatu walikwenda katika kituo hicho kuripoti kuibiwa kwa simu na walianza kujitetea  wakati afisa mmoja wa polisi wa kiume alipojaribu kumvua mmoja wao vazi lake la hijabu na hatimaye wote kupigwa risasi huku mmoja wao akiteketezwa kuficha ukweli kuhusiana na tukio hilo.

"Hakukuwa na silaha, mkanda wa mabomu ama njama yoyote ya kigaidi", yanasema makundi hayo, ambayo ni Muslim for Human Rights, MUHURI, lenye makao yake Mombasa, na Human Rights Watch lenye makao yake jijini New York, Marekani.

"Polisi hutunga habari kuficha makosa"

Mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Shughuli za Polisi, Macharia Njeru, anasema kuwa taarifa hizo zinazotofautiana zimesababisha taasisi yake kuanza uchunguzi kamili. Uchunguzi huo unaweza kusababisha kufunguliwa kwa kesi ya uhalifu, hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa waliohusika ama pia kufutwa kazi kwa maafisa hao.

Nembo ya Human Rights Watch
Human Rights Watch yaishutumu polisi kuficha ukweli

Kulingana na Otsieno Namwaya, mtafiti wa shirika la Human Rights Watch kanda ya Afrika, polisi nchini Kenya hutunga habari za kuficha makosa yao na kutumia ugaidi kuhalalisha mauaji yao yote. Katika kisa hiki, Nyamawaya anasema, kuwa kuna maswali mengi yanayokosa majibu. Inaonekana kuwa polisi wanajaribu sana kutunga maelezo.

Mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI lenya makao yake mjini Mombasa, Khelef Khalifa, alisema kuwa picha za vidio zikimuonesha mmoja wa wanawake hao akiomba dua huku akigaaga chini, baada ya kupigwa risasi, zinathibitisha kuwa hakupata usaidizi wa kimatibabu kwa masaa mawili mazima. Akizungumza na Deutsche Welle mchana wa leo kwa njia ya simu, naibu wa shirika hilo, Hassan Abdi Adel, amesema lazima uchunguzi ufanyike.

Khalifa aliongeza kuwa iwapo wanawake hao wangekuwa magaidi kama inavyodaiwa na polisi, wangekamatwa. Pia alitilia shaka uwezekano wa njama hiyo inayodaiwa, akisema "inatatiza kuwa wasichana  hao walikwenda kuvamia kituo cha polisi wakiwa na kisu. Wasichana hao hawawezi kuiba hata katika nyumba yangu."


Ijumaa iliyopita, mtaalamu wa serikali wa upasuaji wa maiti aliahirisha upasuaji wa miili ya dada hao wawili na siku ya pili wakazikwa. Tangu tukio hilo la Mombasa, polisi wametoa madai mbali mbali, ikiwemo barua iliyoandikwa kwa mkono inayokiri kuwa wanahusika na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, IS, lakini ambayo bado inasubiri kuthibitishwa.

Baada ya shambulizi hilo kuripotiwa, mtandao unahushishwa na IS ulidai kuwa kundi hilo lilifanya mashambulizi hayo. Lakini kwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, madai hayo ni ya kawaida na yatashtua tu watu wasiojuwa wanachokifanya maafisa wa polisi.

Mwandishi: Tatu Karema

Mhariri: Mohammed Khelef