1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Tanzania wataka mabadiliko ya mifumo ya utawala

George Njogopa21 Desemba 2020

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimesema havitajali tofauti zao bali viko tayari kusimama katika jukwaa moja kupigania madai yao ya kudai mabadiliko ya katiba na kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3n11x
Tansania Daressalam | Wahl 2020 | Ibrahim Lupumba, CUF
Picha: Said Khamis/DW

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya chama cha wananchi Cuf kutangaza msimamo wao wa kushirikiana na wadau wa kidemokrasia ikiwamo vyama vya upinzani kuwasilisha kilio kutaka mabadiliko katika mifumo ya kiutawala na uchaguzi.

Hata hivyo, vimeonya kuwa suala la kudai katiba mpya haliwezi kuchukuliwa kama ajenda ya chama fulani cha siasa. 

Vyama hivyo vinaonekana kuweka kando tofauti zao na kuja na msimamo unaofanana pale wanapoona hoja ya mabadiliko ya kidemokrasia inazungumzwa na vyama vyote hivyo ili kutimiza shabaha yao jambo la kushirikiana halikwepeki tena.

Miito ya kutaka katiba mpya Tanzania

Ingawa kwa miaka kadhaa vyama hivyo vimekuwa na kauli moja pindi inapofikia hatua ya kudai mabadiliko ya katiba na tume huru ya uchaguzi, lakini katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mpasuko wa kisiasa miongoni mwa vyama hivyo, na kikubwa zaidi chama cha wananchi cuf kimewahi kushutumiwa na vyama vingine kwa madai ya kutaka kuuwa upinzani.

Miito ya kutaka katiba mpya Tanzania

Hata hivyo, hatua iliyotangazwa na chama cha cuf katika kongamano lao la kudai katiba na tume huru kuwa inafungua milango ya kushirikiana na vyama vingine vya upinzani, inaonekana kuungwa mkono kila upande.

Mkurugenzi wa mawasiliano itifaki na mambo ya nje wa Chadema,John Mrema anaona suala la kudai mabadiliko ya katiba na tume huru haiwezi kuwa ajenda ya wanasiasa bali ni jambo ambalo mizizi yake imejikita kwa wananchi.

Rais John Pombe Magufuli akipiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita Oktoba 28, 2020
Rais John Pombe Magufuli akipiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita Oktoba 28, 2020Picha: REUTERS

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Iringa mjini kupitia tiketi ya chadema, Peter Msingwa mbali ya kuunga mkono hoja ya kuwa na katiba mpya, lakini anaonyesha wasiwasi wake.

Anasema suala la kuwa na katiba mpya ni jambo jema ambalo linapiganiwa na watanzania wengi lakini wakati mwingine baadhi ya vyama hivyo vimekuwa na kile anachokiona hali ya kwenda mbele na kurudi nyuma.

Kilio cha vyama vya upinzani kulalamikia matokeo ya uchaguzi

Akitoa uzeofu wa chama chake katika masuala ya kupigania katiba mpya, mwanasiasa wa siku nyingi wa chama cha NCCR Mageuzi, Sammy Ruhuza amesema kuwa kilio cha vyama vya upinzani kulalamikia matokeo ya uchaguzi, kinaweza kupata mwarubaini wake iwapo mabadiliko yanayopigiwa kulele yatatekelezwa.

Kilio cha upinzani nchini Tanzania

Mkurugenzi wa habari, mawasiliano ya umma na itikati wa cuf, Mohammed Ngulangwa ameiambia DW kuwa chama hicho kiko tayari kushirikiana na vyama vyovyote vya siasa kupigania madai ya katiba mpya.

Ni kwa kiasi gani serikali ya chama tawala CCM inaweza kukubali kurejea mezani kujadiliana na upinzani kuhusiana na madai hayo, na Rais John Magufuli amewahi kukaririwa akisema kuwa suala la katiba mpya halipo kwenye vipaumbele vyake.