1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Ukraine wazidi kuishinikiza serikali

29 Januari 2014

Baada ya kufanikiwa kulishinikiza baraza la mawaziri lijiuzulu hapo jana, leo upinzani nchini Ukraine umeongeza mbinyo kwa serikali wakiitaka iwaachie huru wanaharakati wote walioko jela.

https://p.dw.com/p/1AyqA
Mwandamanaji akiwapigia gita polisi waliojipanga kuzuia maandamano mjini Kiev.
Mwandamanaji akiwapigia gita polisi waliojipanga kuzuia maandamano mjini Kiev.Picha: Reuters

Bunge la Ukraine linatazamiwa kujadiliana hivi leo msamaha kwa waandamanaji, siku moja baada ya Waziri Mkuu Mykalo Azarov na baraza lake zima kujiuzulu, na wabunge kuzifuta sheria zilizokuwa zikiwabana waandamanaji, kwa lengo la kuwaridhisha wapinzani wa serikali.

Matarajio makubwa ni kwamba leo bunge litaridhia kuachiliwa huru kwa watu wanaoshikiliwa kwa sababu ya maandamano yaliyouathiri mji mkuu na miji mingine kadhaa nchini humo.

Kiongozi wa upinzani na bingwa wa zamani wa ndondi duniani, Vitali Klitschko, ameiita Jumatano ya leo kuwa ni siku ya kupambana kwa ajili ya wenzao walioko jela.

"Leo tunataka kulipigania suala moja, suala muhimu sana la msamaha ili kuzuia mashitaka dhidi ya waandamanaji wote. Hili ni muhimu sana." Amesema Klitschko.

Tayari Rais Yanukovych ameshasema kuwa anataka msamaha huo utoke kwa sharti la waandamanaji kuondoka kwenye majengo ya serikali na kuondoa vizuizi vya barabarani.

Juzi Jumatatu waandamanaji waliondoka kwenye jengo la wizara ya sheria, lakini wametoa wito wa kuyakalia majengo mengine yote ya serikali hadi wenzao wote waliokamatwa waachiliwe.

Obama awaunga mkono waandamanaji

Katika hotuba ya jana kwa taifa, Rais Barack Obama wa Marekani aliwaunga mkono waandamanaji nchini Ukraine na kuitolea wito serikali ya Rais Yanukovych kuridhia matakwa yao.

Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia taifa.
Rais Barack Obama wa Marekani akihutubia taifa.Picha: picture-alliance/dpa

"Kwa Ukraine, tunasimamia msingi kwamba watu wote wana haki ya kuelzea mawazo yao kwa uhuru na kwa amani, na kuwa na kauli katika ujenzi wa mustakabali wa nchi yao." Alisema Rais Obama.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani imesema Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, alimpigia tena simu Rais Yanukovych jioni ya jana kumpongeza kwa "maendeleo" yaliyopatikana hadi sasa kwenye mazungumzo na wapinzani, lakini akamshajiisha aendelee kusaka muafaka wa kisiasa, unaohusisha msamaha unaojadiliwa leo bungeni.

NATO yailaumu Urusi

Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, ameilaumu Urusi kwa kuishinikiza serikali ya Ukraine kutosaini mkataba wa mashirikiano na Umoja wa Ulaya, na hivyo kuchochea machafuko yanayoendelea nchini humo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen.Picha: Reuters

Akizungumza na gazeti la Le Figaro la Ufaransa, Rasmussen amesema na hapa namnukuu: "Mkataba wa ushirikiano na Ukraine ungelikuwa hatua kubwa kwenye usalama kati ya Ulaya na Atlantiki. Nasikitika sana kwamba haukuwezekana na sababu inafahamika wazi, ni shinikizo la Urusi."

Licha ya kusisitiza kwamba mashirikiano kati ya NATO na Urusi yameongezeka, lakini Rasmussen alisema kuna tafauti kubwa kwenye masuala kadhaa, hasa la uhasama wa Urusi kwenye nchi za Ulaya ya Mashariki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman