1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wa Syria kuamua kuhusu mazungumzo ya Geneva

27 Januari 2016

Sehemu kubwa ya upande wa upinzani wa Syria wanaendelea na majadiliano yao katika mji mkuu wa Saudi Arabia-Ryadh kuamua kama washiriki katika mazungumzo ya amani ya Geneva, Ijumaa ijayo,au la.

https://p.dw.com/p/1HkXl
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria,Staffan de MisturaPicha: Reuters/D. Balibouse

Akizungumza na shirika la habari la AFP baada ya kuwasili katika hoteli ya fakhari ya mjini Ryadh, mkutano huo unakofanyika, msemaji wa "kamati kuu ya majadiliano"-HNC, Monzer Makhous, amesema mazungumzo yao huenda yakadumu siku nzima.

Wajumbe wa kamati hiyo inayoungwa mkono na Saudi Arabia wameanza kujadiliana tangu jana wakitilia mkazo wao peke yao ndio wanaobidi kuwakilisha upande wa upinzani.

Lakini wawakilishi wa makundi kadhaa mengine ya upinzani ambayo hawawakilishwi katika kamati hiyo,wameliambia shirika la habari la AFP, kwamba wamealikwa pia na Umoja wa Mataifa kushiriki katika mazungumzo Ijumaa ijayo mjini Geneva.

"Jibu litakuwa kupata ufafanuzi na sio kukubali au kukataa," amesema msemaji wa kamati kuu ya majadiliano, Monzer Makhous na kuongeza, "wanataka kujua nani wengine wamealikwa na kwa misingi gani na kipi kitakachojadiliwa."

Masuala ya kiutu ni muhimu kuliko mazungumzo ya kisiasa

Mwanachama mwengine wa kamati hiyo, Salem al Meslat anachambua: "Tunajiandaa vizuri kushiriki katika mazungumzo ya Geneva. Lakini kuna mengi bado, azimio la Umoja wa mataifa nambari 2254, vifungu nambari 12 na 23, kuna masuala ya kiutu, hayo kwetu sisi ni muhimu zaidi kuliko mjadala wowote wa kisiasa."

Syrische Flüchtlinge an jordanischer Grenze
Wakimbizi wa Syria kataika mpaka na JordanPicha: Getty Images/AFP/K. Mazraawi

Ofisi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura imesema imetuma mialiko kwa ajili ya mazungumzo ya Ijumaa ijayo, lakini haikufafanua nani wataiwakilisha serikali ya rais Bashar al Assad wala upande wa upinzani nchini Syria.

Wakurd wa PYD hawatoalikwa mazungumzoni

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema hivi punde amearifiwa na de Mistura kwamba Wakurdi wa chama cha Umoja wa kidemokrasi - PYD hawatoalikwa kuhudhuria mazungumzo ya Geneva.

Syrien Islamistische Kämpfer der Al-Nusra Front
Waasi wa itikadi kali wa Al NusraPicha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa ameongeza kusema amezungumza na msimamizi wa upande wa upinzani Riad Hijab aliyemhakikishia kwamba watashiriki katika mazungumzo hayo - ingawa wanahitaji ufafanuzi kuhusu wale watakaoshiriki na kile kilichotekelezwa upande wa kiutu na pia kuhusu kile kitakachojadiliwa.

Kundi jengine la upinzani - Muungano wa Taifa la Syria linashurutisha kushiriki katika mazungumzo ya Geneva na kuacha kuzingirwa maeneo pamoja na kutekelezwa masharti mengineyo nchini humo. Kundi hilo linasema linasubiri jibu la katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu madai yao kabla ya kutamka kama watashiriki au la mazungumzoni.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/AP

Mhariri: Josephat Charo