1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wa Ukraine ziarani Berlin

17 Februari 2014

Mvutano unaendelea Ukraine huku upinzani ukitafuta usaidizi zaidi nchini Ujerumani kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro uliodumu wiki 12 sasa.Upinzani unataka rais apunguziwe madaraka upate kuunda serikali ya mpito

https://p.dw.com/p/1BAZH
Dmitri Bolatow kiongozi wa vuguvugu la maandamano na Kiongozi wa upinzani Vitali Klitschko
Dmitri Bolatow kiongozi wa vuguvugu la maandamano na Kiongozi wa upinzani Vitali KlitschkoPicha: picture-alliance/dpa

Mvutano na hali ya wasiwasi bado imetanda nchini Ukraine huku upinzani ukimshutumu rais Viktor Yanukovich na washirika wake kwa kuchelewesha mazungumzo yanayoweza kusababisha kuchukuliwa hatua ya rais huyo kupunguziwa madaraka.Wakati huohuo Ujerumani ambayo inabeba dhima kubwa katika kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu imesema kitendo cha kuachiwa huru waandamanaji waliokuwa wamekamatwa pamoja na kuondoka kwa waandamanaji katika ukumbi wa baraza la mji wa Kiev ni cha kutia moyo kwamba serikali na wapinzani wanaweza kufikia msimamo wa pamoja.

Dhima ya Ujerumani

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Martin Schaefer amesema ni jukumu sasa la maafisa wa Ukraine kuzingatia makubaliano ya kukomesha vitenco vya kuwakamata waandamanaji.Matamshi hayo yamekuja ikiwa ni saa chache kabla ya mkutano unaotarajiwa kati ya Kansela Angela Merkel na viongozi wa Upinzani wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk na Vitali Klitschko mjini Berlin.

Kiongozi wa upinzani Ukraine Vitali Klitschko na waziri wa nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Kiongozi wa upinzani Ukraine Vitali Klitschko na waziri wa nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa

Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alikwenda urusi kujaribu kutafuta uungaji mkono wa azimio la amani kuelekea mvutano huu wa Ukraine.Ndani ya Ukraine kwenyewe bado kuna hali ya wasiwasi huku upinzani ukiendelea kumtia kishindo rais Viktor Yanukovich kuridhia madaraka yake yabanwe hatua ambayo inaweza kuupa nafasi upinzani kuunda serikali ya mpito ili kuutanzua mvutano uliodumu wiki 12 zilizoshuhudia ghasia mitaani.

Aidha msamaha uliotangazwa na serikali kwa wanaharakati waliokamatwa wakati wa maandamano ya umma na vurugu umeanza kutekelezwa baada ya waandamanaji kuondoka kwenye ukumbi wa baraza la jiji la kiev pamoja na majengo mengine ya manisapaa katika nchi hiyo .Hata hivyo pamoja na hayo hali ya wasiwasi bado imetanda wakati ambapo upinzani unamtuhumu rais Yanukovich na washirika wake kuyaburuza majadiliano ambayo yanaweza kutowa nafasi ya kumuondolea madaraka yake yanayoangaliwa kama ya kidikteta.

Dhana ya Upinzani

Rais Viktor Janukovitsch azidi kukabiliwa na wakati mgumu
Rais Viktor Janukovitsch azidi kukabiliwa na wakati mgumuPicha: picture-alliance/dpa

Wapinzani wanashuku kwamba rais huyo anajaribu kupunguza kasi ya vuguvugu la upinzani .Hata hivyo kutokana na kuzidi kuporomoka kwa hali ya uchumi na wasiwasi wa kushuka zaidi kwa thamani ya sarafu dhaifu ya nchi hiyo(Hryvnia) rais Yanukovych anazidi kushinikizwa kumtangaza waziri mkuu atakayechukuwa nafasi ya yule aliyekuweko ambaye ni mzaliwa wa Urusi Mykola Azarov aliyemtimuwa Januari 28.Chaguo lake la waziri mkuu mpya huenda likachochea kuingia kwa mikopo mingine chini ya mpango ule wa mkopo wa dola bilioni 15 kutoka Urusi kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kujikwamua haraka kutokana na madeni.

Hata hivyo ikiwa ataipinga miito inayoitisha mageuzi ya kikatiba na badala yake akaamuwa kumtangaza waziri mkuu mwengine wa msimamo mkali kinachotajiriwa huenda ni mitaa ya Ukarine kufurika tena waandamanaji.Kiongozi wa Upinzani anayesubiriwa kukutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakati wowoet kuanzia sasa ameshasema waukraine wamechoshwa kabisa na mfumo wa sasa na kinachofanyika sasa ni kuzidi kutia kishindo kuirudisha katiba ya zamani ambayo itamvuwa madaraka rais ya kuidhibiti serikali na mfumo wa sheria.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman.