1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wafunga ndoa Pakistan

15 Novemba 2007

Mawaziri wakuu 2 wa zamani wa Pakistan wachanganya nguvu zao kwa shabaha ya kumtimua jamadari Musharraf madarakani.Musharraf kuunda leo serikali ya mpito.

https://p.dw.com/p/CEDE
Bhutto afunga ndoa na Sharif
Bhutto afunga ndoa na SharifPicha: AP

Wakati mawaziri wakuu wa zamani wa Pakistan- Benazir Bhutto na Nawaz Sharif, wameafikiana kuunganisha nguvu zao kumtimua madarakani jamadari Musharraf,hasimu yao huyo anatarajiwa kuteua leo serikali ya mpito kusimamia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanywa mwezi januari,mwakani.

Upinzani lakini, umeueleza uchaguzi huo ni aibu chini ya utawala wa kijeshi.

Maafikiano hayo yanaunganisha nguvu za vyama 2 vikubwa kabisa vya upinzani vya mawaziri wakuu wa zamani-Benazir Bhutto na Nawaz Sharif dhidi ya mtawala wa kijeshi jamadari Musharraf.Viongozi hao 2 waliokuwa mahasimu siku za nyuma wamekubaliana kjuzika tofauti zao ili kumpiga vita kwa pamoja jamadari Musharraf hadi pale ameacha madaraka yote 2 –yale ya urais nay a mkuu wa majeshi.Viongozi hao 2 wa upinzani walizungumza kwa simu hiyo jana.

Raja Zafar-ul Haq, mwenyekiti wa Muslim League-chama cha Nawaz Sharif amenukuliwa kusema, “Ametuhakikishia (bibi bhutto) kuendelea na vita dhidi ya jamadari Musharraf hadi amejiuzulu kutoka nyadhifa zake zote mbili.”

Akaongeza Haq kusema kwamba, Musharraf hakubaliki ama rais au hata mkuu wa majeshji.

Chama cha Benazir Bhutto nacho kimethibitisha kuwa viongozi hao 2 walizungumza lakini kiaarifu kitatoa taarifa juu ya mazungumzo yao baadae hii leo.

Wakati bibi Benazir Bhutoo yuko kizuizini nyumbani mwake mjini Lahore,Nawaz Sharif anaongoza upinzani akiwa uhamishoni nchini Saudi Arabia.Bhutto ambae chama chake cha Pakistan Peoples’ Party ndicho chama kikubwa kabisa cha upinzani nchini Pakistan,alikuwa na mazungumzo ya kugawana madaraka na jamadari Musharraf yalioungwamkono na nchi za magharibi kabla Musharraf kutangaza hali ya hatari hapo nov.3.Juzi akafuta uwezekano wowote wa mazungumzo zaidi na Musharraf na akaapa kutotumika kabisa chini ya Musharraf.

Benazir Bhutto alikuwa waziri mkuu wa Pakistan mara 2-kwanza kutoka 1988 hadi 1990 na tena kutoka 1993 hadi 1996.Baina ya kipindi hicho mpinzani wake Nawaz Sharif alikuwa waziri mkuu na akashika wadhifa huu tena 1996 hadi 1999 alipoangushwa madarakani na jamadari Musharraf.

Ushirika wa kwanza kati ya Benazir Bhutto na Nawaz Sharif ulivunjika kutokana na Bhutto kuwa na mawasiliano na jamadari Musharraf.

Wakati Bhutto na Sharif wanafunga ndoa mpya, jamadari Musharraf anakaza kamba:Anatarajiwa leo kuunda serikali ya mpito itakayoiongioza Pakistan katika uchgaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Januari,mwakani.

Marekani na washirika wake wengine wakidai hatua kuchukuliwa haraka kurejesha demokrasi nchini Pakistan-dola la kiislamu lenye kumiliki silaha za kinuklia-jamadari Musharraf ameahidi kuitisha uchaguzi Januari 9,lakini hakubainisha ni lini katiba itarudi kufanya kazi wala hakudhukuru ni lini hali ya hatari itakoma.

Vyama vya upinzani vinasema, uchaguzi chini ya tangazo la hali ya hatari ni aibu na ni kibri.