1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno mbioni kutuliza hofu za wawekezaji

27 Aprili 2010

Ureno ipo mbioni kujaribu kuondosha hofu za masoko ya fedha kuwa nchi hiyo huenda ikafuata nyayo za Ugiriki iliyokumbwa na madeni makubwa na ikatumbukia katika matatizo ya kifedha.

https://p.dw.com/p/N7S4
Jul 25, 2008 - Lisbon, Portugal - Portugal's President, ANIBAL CAVACO SILVA, addresses journalists at the end of the 7th Community of Portuguese Language Countries (CPLP) Summit held at the Belem Cultural Center in Lisbon, Portugal. The CPLP is a forum for friendship among Portuguese-speaking nations where Portuguese is the official language which gathers more than 220 million people across the globe +++(c) dpa - Report+++
Rais wa Ureno, Anibal Cavaco Silva.Picha: picture-alliance/ dpa

Kwa kweli kifedha Ureno ipo katika hali bora kuliko Ugiriki, lakini kuna wasiwasi kuwa mzozo wa Ugiriki huenda ukaathiri nchi zilizokuwa na uchumi dhaifu katika kanda inayotumia sarafu ya Euro. Wasiwasi huo umezidi baada ya serikali ya Ugiriki kuomba msaada kutoka Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF Ijumaa iliyopita.

Hofu hizo zimeshaanza kuathiri masoko ya hisa nchini Ureno ambako mwanzoni mwa wiki hii, hisa ziliporomoka kwa zaidi ya asilimia 3. Wakati huo huo, riba inayotozwa na wawekezaji kwa hati za serikali ya Ureno za muda wa miaka 10, imevuka asilimia 5. Hiyo humaanisha kuwa sasa huigharimu serikali pesa zaidi kupata mikopo katika masoko ya fedha.

Kwa mujibu wa Paul de Grauwe,mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Ureno itajikuta katika hali ngumu ikiwa wadadisi wana wasiwasi na uwezo wa nchi hiyo kukabiliana na matatizo yake ya fedha. Mtaalamu huyo wa Kibeligiji amesema, hali ya Ureno si mbaya kama ile ya Ugiriki lakini hiyo haitoshi kutuliza wasiwasi wa wawekezaji katika masoko ya fedha.

Mwaka uliopita,nakisi ya bajeti ya serikali ya Ureno ilivunja rekodi ilipoongezeka hadi asilimia 9.4 ya pato jumla la taifa na hivyo deni lake lilifikia Euro bilioni 126. Hiyo ni sawa na asilimia 76.6 ya pato jumla la taifa. Mambo ni mabaya zaidi huko Ugiriki,ambako katika mwaka 2009, nakisi yake ya bajeti ilifikia asilimia 13.6 na deni lake lilipindukia Euro bilioni 273 sawa na asilimia 115.1 ya pato jumla la taifa.

Juma lililopita, serikali ya kisoshalisti nchini Ureno ilipendekeza mpango unaodhamiria kupunguza matumizi yake. Azma ni kushusha nakisi ya bajeti hadi asilimia 8.3 ya pato jumla la ndani katika mwaka huu wa 2010. Na mwaka 2013 inatazamia kuishusha chini ya kiwango kinachotakiwa na Umoja wa Ulaya cha asilimia 3.

European Commission President, Jose Manuel Barroso addresses reporters during a news conference after his reelection at the European Parliament in Strasbourg, eastern France, Wednesday, Sept. 16, 2009. The European Parliament gave Barroso another five-year term as European Commission president Wednesday, but its vote reflected lingering misgivings about the conservative ex-Portuguese premier in the EU assembly. (AP Photo/Christian Lutz)
Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso.Picha: AP

Hata Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya,Jose Manuel Barroso, ameihimiza serikali ya Ureno kuchukua hatua kali za kupunguza matumizi. Akisisitiza kuwa Ureno inakabiliwa na wakati mgumu, Barosso aliekuwa waziri mkuu wa zamani wa kihafidhina nchini Ureno,alitoa mwito kwa serikali,upande wa upinzani na umma kuonyesha wajibu wao.

Serikali ya Ureno inatazamia kuwasilisha bungeni hatua za mwanzo za mpango wa kupunguza matumizi yake. Katika jitahada ya kuwatuliza wananchi na masoko ya fedha,Rais Anibal Cavaco Silva alisisitiza kuwa Ureno haikabiliwi na hatari ya kufilisika.

Mwandishi: Martin,Prema/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed