1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ureno nayo yafuata nyayo za Uhispania kubana matumizi

Kabogo Grace Patricia14 Mei 2010

Hatua hiyo ya Ureno ni kwa lengo la kupunguza nakisi ya bajeti yake ili kujiepusha na mzozo wa madeni.

https://p.dw.com/p/NNSO
Waziri Mkuu wa Ureno, Jose Socrates.Picha: AP

Baada ya serikali ya Uhispania kutangaza mipango ya kupunguza mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma ili kuimarisha hatua za kukabiliana na kuongezeka nakisi katika bajeti yake, Ureno nayo imetangaza mpango wa kubana matumizi ili kupunguza nakisi ya bajeti yake, ili kujiepusha  na mzozo wa madeni.

Serikali ya Kisoshalisti ya Ureno imetangaza kuwa miongoni mwa hatua itakazozichukua ni kuongeza kodi, kupunguza mishahara na kusitisha miradi mikubwa ya umma kama vile ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Lisbon. Waziri Mkuu wa Ureno, Jose Socrates, amesema lengo la nchi hiyo kuchukua hatua hizo ni kupunguza nakisi katika bajeti yake ya asilimia 9.4 la pato la ndani hadi kufikia asilimia 5.1 hapo mwakani.

Taarifa zinaeleza kuwa mishahara ya mawaziri, wabunge, maafisa wa ndani na wakuu wa makampuni ya umma, itapunguzwa kwa asilimia 5. Vyombo vya habari nchini humo vimeeleza kuwa hatua hizo za serikali ni za kushtua

Ureno ikiwa kama mwanachama wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro, inatakiwa kushikilia nakisi yake ya mwaka chini ya asilimia 3.0 ya pato lake. Ureno na Uhispania kama ilivyo kwa Ugiriki, zinapambana kuimarisha uchumi wao. Waziri Mkuu huyo wa Ureno amesema kodi ya mauzo itapandishwa kwa asilimia 1 na hivyo kufikia asilimia 21. Wakati hayo yakijiri, umoja wa vyama vya wafanyakazi nchini Uhispania vimeitisha mgomo ikiwa ni katika kupinga mpango wa serikali wa kupunguza mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma.

Wakati nchi hizo zinachukua hatua za kupambana na mzozo wa madeni, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ameonya kuwa nchi zote za Umoja wa Ulaya zinaweza kuwa katika kitisho iwapo sarafu ya Euro itaachiwa itetereke kutokana na mzozo wa madeni. Baada ya mzozo wa madeni nchini Ugiriki, tahadhari ya kimataifa sasa imezigeukia Ureno na Uhispania.

Tangazo la Ureno limekuja baada ya Waziri Mkuu wa Uhispania, Jose Luis Rodriguez Zapatero kusema jana kwamba serikali yake itapunguza mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma kwa asilimia 5 na kupunguza matumizi katika sekta ya uwekezaji na pensheni.

Wachambuzi wengi wa masuala ya kiuchumi wanasema kuwa sarafu ya Euro bado iko katika matatizo kwa sababu mzozo wa madeni nchini Ugiriki umeongeza wasi wasi katika mataifa yote ya Umoja wa Ulaya. Kwa upande mwengine, Benki Kuu ya Australia imeonya kuwa mzozo wa kiuchumi barani Ulaya unaweza kusababisha matatizo katika ukuaji uchumi wa bara la Asia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman