1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kuendelea na mashambulizi Aleppo

29 Septemba 2016

Urusi imesema inaendelea mbele na kampeni yake ya mashambulizi nchini Syria leo licha ya onyo la Mrekani kwamba itasitisha mazungumzo kuhusu mzozo wa nchi hiyo ikiwa Urusi haitakomesha mashambulizi mjini Aleppo.

https://p.dw.com/p/2Qk69
Syrien Aleppo Menschen zwischen Trümmern
Picha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Urusi imeapa kuendelea na mashambulizi yake nchini Syria huku maafisa wa Marekani wakitafuta hatua kali muafaka dhidi ya uamuzi wa Urusi kupuuzilia mbali mchakato wa amani na kutafuta ushindi wa kijeshi kwa niaba ya rais wa Syria, Bashar al Assad. 

Urusi na Syria zilianza mashambulizi ya kulikomboa eneo la Aleppo linalodhibitiwa na waasi mwezi huu, na hivyo kuyavunja makubaliano ya wiki moja ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa katika vita vilivyodumu karibu miaka sita. Msemaji wa utawala wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesisitiza kwamba Urusi bado inataka kuona makubaliano na Marekani ya kusitisha mapigano Syria yakifaulu, lakini akasema Marekani imeshindwa kutimiza ahadi zake.

Umoja wa Mataifa umeelezea leo hali ya kukatisha tamaa katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi mashariki ya Aleppo, ukionya kwamba mamia ya Wasyria wanatakiwa kuhamishwa wakihitaji matibabu na kwamba kuna chakula cha kutosha asilimia 25 ya wakaazi jumla wa mji huo. 

Syrien Zerstörung in Aleppo
Madaktari wakikagua uharibifu katika hospitali ya kitongoji cha al-Maadi, AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

Naibu mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Syria, Ramzy Ezzeldin Ramzy, amesema watu wapatao 600 wamejeruhiwa katika mji uliozingirwa wa Aleppo na wananyimwa mahitaji muhimu ya matibabu. Ramzy amezitaka Urusi na Marekani kuyafufua tena makubaliano ya kusitisha mapigano, akisema ndio njia muafaka ya kupata suluhisho kwa hali ngumu inayowakabili raia wa Syria.

"Mashambulizi ya mabomu sharti yakome, raia walindwe na usitishaji mapigano urejeshwe tena. Tunasisitiza tena miito iliyotolewa mara kwa mara na Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili. Tunawataka wenyekiti wa kundif la kimataifa linaloisadiaia Syria kufanya kazi pamoja kuhakikisha usitishaji mapigano unarejea tena."

Akizungumza mjini Geneva baada ya mkutano wa kikosi cha utoaji misaada ya kibinadamu kinachaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Ramzy amesema kitu cha muhimu sasa ni kushughulikia kwa haraka suala la matibabu. Hospitali nyingi zimeharibiwa katika mashambulizi ya kutokea angani na dawa zimepungua, huku majeruhi wakikosa matibabu wanayoyahitaji. 

Elsayed Ramzy Ezzeldin Ramzy
Ramzy Ezzeldin Ramzy, Naibu wa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, SyriaPicha: AP

Kwa upande mwingine, Uturuki imesema iko tayari kushirikiana na Urusi kuhusu suala la usitishaji mapigano na utoaji misaada. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amewambia waandishi wa habari leo mjini Ankara kwamba Uturuki imeyajadili masuala hayo na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Iran, Mohammed Javad Zarif.

"Baada ya mahusiano yetu kurejea katika hali ya kawaida, tunajadilina kuhusu masuala haya haya na Urusi. Kama Urusi inataka kushirikiana nasi upande wa usitishaji mapigano na usambazaji wa misaada ya kibinadamu, sisi tuko tayari kabisa."

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wamesema leo kwamba Urusi ina jukumu maalumu kutuliza machafuko na kuupa nafasi mchakato wa kisiasa nchini Syria. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya kansela Merkel, viongozi hao wamekubaliana katika mazungmzo kwa njia ya simu kwamba harakati inayofanywa na utawala wa Syria dhidi ya mji wa Aleppo imezidisha mateso kwa raia.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/rtre/ape
Mhariri: Mohammed Khelef