1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaanza kupunguza idadi ya wanajeshi Syria

Sylvia Mwehozi
6 Januari 2017

Urusi imesema leo kuwa imeanza kupunguza idadi ya wanajeshi wake nchini Syria, chini ya masharti ya mpango tete wa kusitisha mapigano uliofikiwa kati ya makundi ya upinzani na serikali ya Syria

https://p.dw.com/p/2VPqa
Syrien Aleppo Russische Soldaten
Picha ikiwaonyesha wanajeshi wa Urusi wakilinda doria mjini AleppoPicha: picture-alliance/AP/Russian Defense Ministry

Wakati hayo yakiarifiwa ndege za kivita za serikali ya Syria zimeyashambulia kwa mabomu wilaya muhimu inayoshikiliwa na waasi ambayo ni mji mkuu wa chanzo cha maji. 

Rais wa Urusi Vladmir Putin alitangaza kusitishwa kwa mapigano mwishoni mwa mwezi Desmba mwaka jana na kusema kwamba nchi yake itayaondoa baadhi ya majeshi yake kutoka Syria , ambako uingiliaji wake kijeshi umemsaidia Rais Bashar al-Assad.

Mkuu wa Jeshi la Urusi Valery Gerasimov amesema wameanza leo kuondosha manowari zake kutoka mashariki mwa bahari ya Mediterenia zinazoongozwa na meli ya kubebea ndege ya Admiral Kuznetsov. "Usitishaji mapigano katika maeneo yote ndani ya Syria kulianza tangu usiku wa Desemba 30 mwaka jana lakini hakuhusishi makundi ya kigaidi ya kimataifa. Kwa mujibu wa uamuzi wa Amiri jeshi mkuu Rais Vladimir Putin, wizara ya ulinzi inaanza kupunguza vikosi vyake nchini Syria."

Mittelmeer Russischer Flugzeugträger Admiral Kusnezow OVERLAY
Meli ya kubeba ndege za kivita ya Admiral Kuznetsov Picha: picture-alliance/AP/Russian Defe

Meli hiyo iliongoza kupelekwa kwa jeshi la majini la Urusi katika operesheni za pwani ya Syria, ikiwa ni nadra sana kuonekana tangu kuanguka kwa muungano wa kisovieti katika kutoa msaada kwa jeshi la Syria. Mashambulizi ya kiwango kikubwa kwa vikosi vya waasi yalianzishwa kutoka katika manowari tangu mwezi Novemba.

Mkuu wa jeshi la Syria luteni Jenerali Ali Abdullah Ayoub ameitembelea meli hiyo kuhitimisha ujumbe wake. Katika hotuba yake iliyorushwa kupitia televisheni ya taifa ya Urusi, amesisitiza umuhimu wa usaidizi wa jeshi la Urusi kwa Damascus "katika vita dhidi ya ugaidi na hitaji la kuzidisha ushirikiano wa kijeshi" na Urusi hata baada ya "ushindi dhidi ya magaidi."

Wakati hayo yakijiri ndege za kivita za serikali nchini Syria zimeishambulia kwa mabomu wilaya inayodhibitiwa na waasi ambayo ni eneo kuu la chanzo cha maji wakati pande hasimu zikilaumiana kwa kukata njia kuu ya usambazaji.

Syrien Assad Regime verletzt Waffenruhe in Aleppo
Raia wa Syria akikagua eneo baada ya kuharibiwa na ndege za kivita za SyriaPicha: picture alliance/dpa/AA/A. al Ahmed

Damascus imekuwa bila maji kutoka Wadi Barada, tangu Desemba 22 na kuwaacha watu milioni 5.5 wakikosa huduma hiyo.

Umoja wa Mataifa ulionya hapo jana kwamba kuharibu vyanzo vya maji  ni uhalifu wa kivita. Na huko kaskazini mwa Syria jeshi la Uturuki limewaua wapiganaji 32 wa Dola la Kiislamu IS katika shambulio la hivi karibuni.

Uturuki ilianzisha operesheni za kijeshi zaidi ya miezi minne iliyopita ili kuwafurusha wapiganaji wa IS kutoka mpakani mwake na kuwazuia wanamgambo wa kikurdi kuzidi kuijpanua.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga