1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani hazielewani kuhusu makombora ya kinga

P.Martin18 Machi 2008

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice na Waziri wa Ulinzi Robert Gates wamekutana na mawaziri wenzao wa Urusi mjini Moscow.Lakini wataalamu wanahofia mkutano huo hautokuwa na matukio yenye umuhimu mkubwa.

https://p.dw.com/p/DQXK
Condoleezza Rice, left, listens as Russian Foreign Minister Sergei Lavrov.jpg U.S. Secretary of State Condoleezza Rice, left, listens as Russian Foreign Minister Sergei Lavrov speaks during the talks in Moscow, Russia, Tuesday, March 18, 2008.U.S. Secretary of State Condoleezza Rice and Defense Secretary Robert Gates visit Russia for talks at a time of rising tension between Washington and Moscow over U.S. missile defense plans.(AP Photo/Sergey Ponomarev)
Wazairi wa Nje wa Marekani Condoleezza Rice (kushoto)na Waziri wa Nje wa Urusi Sergei Lavrov wakati wa majadiliano yao mjini Moscow.Picha: AP

Majadiliano ya mawaziri Rice na Gates pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov na Waziri wa Ulinzi Anatoly Serdyukov yamehusika na masuala ya usalama, kama ushirikiano katika sekta ya nyuklia kwa matumizi ya amani,kuzuia usambazaji wa silaha za maangamizi na kupiga vita ugaidi.Hata mada zinazohusika na usalama wa kimataifa na katika kanda hiyo zilikuwemo katika ajenda ya mazungumzo yao.Oktoba mwaka jana viongozi hao wanne walipokutana mjini Moscow,walishindwa kuafikiana juu ya mpango wa makombora ya kinga.Kwa hivyo,wachambuzi wanahofia kuwa hakuna kipya kitakachopatikana,hasa kwa vile Rais George W.Bush anaondoka madarakani mwisho wa mwaka huu.Hata hivyo,wataalamu wa kijeshi wanasema,mashauriano ya kidiplomasia kati ya Urusi na Marekani huenda yakasaidia kwa kiwango fulani, kupunguza tofauti za maoni kati ya pande hizo mbili hasa kuhusu mpango wa Marekani kuweka makombora ya kinga nchini Poland na Jamhuri ya Czech.

Kwa maoni ya Jemadari Viktor Yesin,ambae hapo zamani alikuwa mkuu wa mkakati wa makombora ya Urusi, suluhisho la mgogoro huo ni kuanzisha kituo cha pamoja kubadilishana habari muhimu yaani kuzindua mfumo wa kuonya mapema kama ilivyo pendekezwa na Marekani na Urusi katika mwaka 2000.Mpango huo ungesaidia kuanzisha mfumo wa kimataifa utakaodhibiti usambazaji wa teknolojia ya makombora na vile vile utasaidia kuondosha hatari ya kurusha makombora kwa makosa.

Lakini ripoti za vyombo vya habari zinasema,Marekani huenda ikaamua kuweka rada za kugundua makombora nchini Uturuki badala ya Ulaya ya Mashariki na hivyo kupunguza mvutano unaohusika na makombora hayo.

Hata hivyo,kuna masuala mengine pia yaliyo na umuhimu kwa pande zote mbili.Kwa mfano kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia.Hivi karibuni Marekani ilifurahi,Urusi ilipopiga kura kuunga mkono pendekezo lililotolewa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York,kuiwekea Iran vikwazo vipya.

Waziri Condoleezza Rice ameitumia fursa ya ziara hii vile vile kukutana na viongozi wa makundi ya kirai yanayoipinga serikali ya Moscow na vile vile wanaharakati wa haki za binadamu kama ilivyo desturi yake anapokuwa ziarani nchini Urusi.Leo asubuhi kabla ya mkutano wake na viongozi hao Rice alisema,atajaribu kutafauta njia ya kusaidia kuleta uwazi zaidi katika mfumo wa kisiasa nchini humo.Waziri Rice mara kwa mara amesema,Kremlin ina usemi mkubwa mno na vile vile serikali ya Rais Vladimir Putin anaeondoka madarakani,imepunguza uhuru wa kidemokrasia nchini Urusi.