1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zimeanza mazungumzo juu ya makombora ya usalama

12 Oktoba 2007

Marekani na Urusi zinafanya mazungumzo ambayo Washington ina azma ya kusisitiza juu ya mpango wake wa kuweka makombora ya usalama kataika nchi za Ulaya ya Mashariki.

https://p.dw.com/p/C7hx
Rais Vladimir Puttin wa Urusi
Rais Vladimir Puttin wa UrusiPicha: AP

Rais Vladimir Puttin ameanza kwa kuionya Marekani kwamba Urusi haitasita kuuvunja mkataba wa makombora ya kinyuklia na wakati huo huo ameitaka Washington iachane na mpango wake wa kutaka kuwekeza makombora ya usalama katika nchi za Ulaya ya Mashariki.

Rais Puttin ameyasema hayo mara baada ya kuanza mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice na mwenzake wa Ulinzi Robert Gates ambao wanafanya ziara nchini Urusi kujadili pendekezo hilo la Marekani na pia kuhusu pingamizi za Kremlin juu ya swala hilo la kuwekeza makombora ya usalama.

Moscow inaupinga mpango huo wa Marekani wa kutaka kuweka makombora mapya ya usalama katika nchi za Poland na Jamuhuri ya Czech.

Rais Vladimir Puttin ametoa tahadhari kwa Marekani juu ya kufanya haraka ya kutekeleza mpango wake huo huku nchi hizo zikiwa bado zinajadiliana.

Urusi inasema kuwa mpango huo wa kuwekezwa makombora ya Radar katika nchi hizo za Ulaya Mashariki unatishia usalama wake na wakati huo huo inahoji kwa nini Marekani isitumie Radar ya kutoa tahadhari ya Urusi iliyoko nchini Azerbaijan?.

Lakini Marekani inakanusha wasiwasi huo wa Urusi kwa kutetea mpango wake kuwa unalenga kujilinda na vitisho kutoka Iran na Korea Kaskazini.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema kwamba katika mazungumzo hayo ya siku mbili Marekani na Urusi pia zitajadili juu ya mpango wa nyuklia wa Iran na uhuru wa jimbo la Kosovo.

Lakini wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kuwa Marekani haitafua dafu kuishawishi Urusi ikubali pendekezo la nchi za magharibi linalotaka Iran iwekewe vikwazo zaidi na baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice amesema ana matumaini kuwa Urusi itaunga mkono vikwazo hivyo dhidi ya Tehran.

Kuhusu uhuru wa jimbo la Kosovo, Urusi inaunga mkono Serbia dhidi ya nchi za magharibi zinazopendelea jimbo la Kosovo lililojitenga ambalo kwa sasa linasimamiwa na umoja wa mataifa lijitawale.

Muda wa mwisho wa mzungumzo kati ya Belgrade na Pristina wa Desemba kumi unakumbushia vipi suluhisho la uhuru wa Kosovo linavyo hitaji kufikiwa kwa haraka.

Marekani na washirika wake wa NATO pia wanakabiliwa na muda mwingine wa mwisho wa Desemba 12 ambapo Urusi imesema itasimamisha mchango wa majeshi yake iwapo nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya magharibi hazitakuwa zimetia saini mkataba wa nchi za Ulaya juu mchango wa wanajeshi wa kawaida.

Mkutano huo pia unahudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa ulinzi Anatoly Serdyukov.