1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na nchi za magharibi Zinakaripiana kuhusu Ukraine

30 Aprili 2014

Urusi na Marekani zinazidi kukaripiana kuhusu mzozo unaozidi makali wa Ukraine huku wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wakiendelea kuyadhibiti majumba ya serikali mashariki ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1BrES
Waasi wanaoelemea Urusi wakipiga doria nje ya jengo la serikali huko HorlivkaPicha: picture-alliance/dpa

Rais Vladimir Putin ameonya vikwazo vya Marekani dhidi ya Moscow vitadhuru masilahi ya nchi za magharibi katika sekta ya nishati nchini Urusi,inayolaumiwa na nchi za magharibi kuchochea mvutano mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu vita baridi kumalizika.

Amekanusha kwa mara nyengine tena kuhusika wanajeshi wa Urusi katika mzozo wa Mashariki ya Ukraine.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameituhumu Urusi kutaka kubadilisha ramani ya usalama Ulaya ya Mashari.Ameitaka Moscow "iihame Ukraine kwa amani" na kuahidi " kila inchi ya ardhi ya jumuia ya kujihami ya NATO italindwa.

Waasi wanadhibiti maeneo zaidi

Wakati huo huo vurugu zinaendelea katika eneo la mashariki la Ukraine,wanamgambo wanaoelemea upande wa Urusi wanaikalia zaidi ya miji 12 ya mashariki hivi sasa.Wamekiteka kituo cha polisi cha Lugansk baada ya mapigano makali yaliyoshuhudia gesi za kutoa macho na risasi kutumika.Wameiteka pia ofisi ya meya huko Gorlivka.Wanadhibiti pia vituo muhimu ikiwa ni pamoja na idara za upelelezi katika miji hiyo.

Proukrainische Demo in Donetsk, 28.04.2014
Maandamano kuunga mkono Umoja wa UkrainePicha: DW

Mjini Kiev rais Olexandre Tourtchinov amekosoa "uzembe" na uhaini" wa vikosi vya kulinda amani katika kuhifadhi mali ya umma na wananchi katika maeneo ya mashariki ya Ukraine.Wasi wasi kama huo unasikika pia miongoni mwa jamii.Maandamano yamepangwa kuitishwa leo mbele ya bunge mjini Kiev kulalamika dhidi ya viongozi kukaa kimya katika mzozo wa mashariki ya Ukraine.Maandamano kuunga mkono Umoja wa Ukraine yamepangwa pia kuitishwa leo usiku huko Donetsk.

Matumaini ya kuachiwa huru wasimamizi wa OSCE

Ama kuhusu wasimamizi wa jumuia ya usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE wanaoshikiliwa tangu ijumaa iliyopita mashafiki ya Ukraine,matumaini yamechomoza huenda wakaachiliwa huru haraka.Msemaji wa jumuia hiyo amesema leo hii huko Slaviansk "mazungumzo yanaendelea vizuri na wanataraji yataleta tija."

OSZE Ukraine Mission Tim Guldimann
Mwakilishi wa tume ya jumuia ya OSCE nchini Ukraine Tim GuldimannPicha: picture-alliance/dpa

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo