1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya anga ya Urusi yanaendelea Syria

4 Novemba 2015

Urusi imesema imeanzisha ushirikiano na makundi ya upinzani nchini Syria, yanayopingana na serikali ya Rais Bashar al-Assad na kufanikiwa kuyashambulia maeneo kadhaa ya magaidi kwa kutumia taarifa zao

https://p.dw.com/p/1GzGF
Ndege ya kivita ya Urusi
Ndege ya kivita ya UrusiPicha: Reuters/Ministry of Defence of the Russian Federation

Mashambulizi hayo yamefanyika huku Marekani ikisema marubani wake wamewasiliana na maafisa wa jeshi la anga la Urusi, hiyo ikiwa ishara kuwa mataifa hayo makubwa yanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha yanamaliza vita vya wenyewe nchini Syria.

Hii ni mara ya kwanza kwa Urusi kukiri kufanya kazi na makundi pinzani kwa Rais Assad, tangu ilipoanzisha mashambulizi yake ya anga nchini Syria. Ndege za kivita za Urusi jana zilishambulia maeneo 24 ya magaidi nchini Syria, ikiwemo kambi za kijeshi, maghala ya silaha na mizinga ya kudungulia ndege.

Rais Bashar al-Assad
Rais Bashar al-AssadPicha: picture alliance/dpa/Sana Handout

Afisa mwandamizi wa jeshi la Urusi, Jenerali Andrei Kartapolov amesema mashambulizi hayo yamefanyika kwa msaada na ushirikiano wa vikosi vinavyopingana na utawala wa Rais Assad, bila ya kufafanua zaidi kuhusu makundi hayo pinzani.

Urusi pia imesema imeandaa mkakati wa kushirikiana na makundi yenye msimamo wa wastani kwa lengo la kupambana na kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS. Wizara ya ulinzi ya Urusi imethibitisha kuhusu ushirikiano wao na wapinzani wa Assad, ikisema ni wenye tija katika kupambana na ugaidi na kuimarisha mchakato wa kisiasa.

Saa chache baada ya kufanyika mashambulizi hayo, wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema marubani wake waliwasiliana moja kwa moja na marubani wa ndege za kivita za Urusi katika anga ya Syria, hilo likiwa jaribio la kwanza na mkakati mpya wa kuhakikisha operesheni za kijeshi za nchi hizo mbili haziingii katika mvutano.

Urusi na Marekani zashiriki mafunzo ya pamoja

''Leo vikosi vya anga vya Urusi na Marekani vimeshirikiana katika mafunzo ya pamoja. Katika mchakato wa mafunzo, tumefanya mazoezi ya kubadilishana taarifa kati ya timu za uendeshaji na udhibiti kwenye kituo cha anga cha Urusi cha Hmeymim na kituo cha kimkakati na operesheni za anga cha Marekani huko Qatar,'' alifafanua Kartapolov

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrow
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei LavrowPicha: Reuters/M. Shemetov

Oktoba 20, Marekani na Urusi zilisaini makubaliano ya kuweka masharti kuhakikisha ndege zao za kivita haziingiliana katika anga, baada ya kuwepo matukio kadhaa yanayoashiria migongano kwenye anga ya Syria.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov leo anatarajiwa kukutana na Mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura mjini Moscow.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi, Maria Zakharova, amesema ajenda kuu itakuwa mchakato wa kisiasa nchini Syria na kuanza kwa mazungumzo halisi kati ya serikali ya Syria na makundi ya upinzani.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/AA

Mistura ambaye alizuru Syria hivi karibuni ametoa wito wa kuwepo juhudi za kidiplomasia kwa serikali ya Syria pamoja na makundi ya waasi kujumuishwa katika mazungumzo yajayo ya kusitisha mapigano nchini humo.

Hata hivyo, Marekani imesema ni mapema mno kwa serikali ya Urusi kuyaalika makundi ya upinzani nchini Syria, kushiriki katika mazungumo ya Urusi. Awali Urusi, ilisema maafisa wa serikali na wapinzani watakutana mjini Moscow wiki ijayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Daniel Gakuba