1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Syria afanya ziara ya kushtukiza Urusi

21 Oktoba 2015

Rais wa Syria Bashar al Assad amefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu vita kuanza nchini mwake kwa kuzuru Urusi ambako amemuambia mwenyeji wake kampeni ya kijeshi aliyoianzisha Syria imesaidia kuudhibiti ugaidi

https://p.dw.com/p/1GrPL
Picha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Druzhinin

Rais Assad amemuambia mwenyeji wake Rais Putin wakiwa mjini Moscow kuwa ugaidi ambao ulikuwa umesambaa nchini mwake na kanda hiyo ungeendelea kusambaa kwa maeneo mengine makubwa iwapo Urusi haingechukua hatua na maamuzi ya kuusaidia utawala wake kijeshi mwezi uliopita na kumshukuru kwa kuunga mkono utawala wake.

Putin kwa upande wake ameahidi kuendelea kuiunga mkono Syria huku akitaka kuwepo suluhisho la kisiasa linaloyajumuisha makundi yote kujaribu kuvimaliza vita ambavyo vimedumu kwa miaka minne.

Urusi itaisaidia Syria

Putin ameongeza kuwa wako tayari kuisaidia Syria sio tu wakati wa mapambano dhidi ya ugaidi, bali hata wakati wa mchakato wa kisiasa. Assad amesisitiza kuwepo umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua za ziada za kisiasa kuutafutia ufumbuzi mzozo nchini mwake.

Rais wa Syria Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow
Rais wa Syria Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini MoscowPicha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Druzhinin

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema nchi yake itaendelea kuupa utawala wa Assad alioutaja halali msaada wa kijeshi kupambana dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS.

Msemaji wa ikulu ya Rais wa Urusi Dmitry Peskov ameitaja ziara hiyo fupi ya Assad kama ya kikazi na kufikia leo asubuhi, Assad alikuwa amesharejea Damascus.

Kiongozi wa Urusi amesisitiza ni raia wa Syria tu ndiyo wanaoweza kuamua mustakabali wa siku za usoni wa taifa lao kupitia mchakato wa kisiasa unaoyashirikisha makundi ya kisiasa, kidini na kikabila utakaoleta suluhisho la kudumu.

Uturuki yasisitiza Assad aondoke madarakani

Hata hivyo Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema kipindi cha mpito nchini Syria kinahitajika ambacho kitahakikisha utawala wa Rais Assad unaondoka madarakani na kusisitiza hakuna kilichobadilika katika msimamo wa Uturuki kuwa utawala wa Assad umepoteza uhalali wake.

Urusi ilianzisha mashambulizi ya kijeshi ya angani mnamo tarehe 30 mwezi uliopita yakiwa mashambulizi ya kwanza ya kijeshi nje ya zilizokuwa nchi za kisoviet kufanywa na nchi hiyo tangu ilipoivamia na kuikalia Afghanistan mwaka 1979.

Kiasi ya watu 250,000 wameuawa tangu vita vya Syria kuanza mwezi Machi mwaka 2011 na nusu ya idadi ya wa Syria wameachwa bila ya makaazi huku mamilioni wakilazimika kuwa wakimbizi.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa

Mhariri:Josephat Charo