1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaendelea kushambulia Syria

Admin.WagnerD15 Oktoba 2015

Watu 10 wameuwawa Alhamisi (15.10.2015)wakati ndege za kivita za Urusi ziliposhambulia katikati ya Syria ambapo kuna mapigano makali yanayoendelea kati ya vikosi vya serikali na waasi wa nadharia kali za Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1GolI
Ndege ya kivita ya Urusi nchini Syria.
Ndege ya kivita ya Urusi nchini Syria.Picha: picture-alliance/dpa/RIA Novosti/D. Vinogradov

Urusi imefanya zaidi ya mashambulizi ya anga 15 kuanzia alfajiri leo hii kwenye viunga vya mji wa Talbisseh na Teir Maaleh kwenye kingo za kaskazini za jimbo la kati la Holms.

Kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza waasi sita ni mongoni mwa watu waliouwawa. Kiongozi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba kwenye medani ya mapambano vikosi vya serikali vikishirikiana na washirika wao vinajaribu kuutenganisha mji mkuu wa Holms na viunga vyake kwa kujaribu kuyavamia meeneo ya kusini ya Talbisseh yanayoshikiliwa na waasi.

Pia ameongeza kusema kwamba vikosi vya Rais Basher Assad vinavyosaidiwa na Urusi pia vinajaribu kuiteka barabara kuu inayotokea Holms kuelekea katika jimbo la kati la Hama.

Waasi wanaopambana dhidi ya serikali

Vikosi vya serikali ya Syria vikisaidiwa na wapiganaji wa kundi la Hezbollah la Lebanon pamoja na mashambulizi ya anga ya Urusi wamepiga hatua ndogo kuelekea kwenye medani ya vita ya barabara hiyo ya kilomita 130 kaskazini mwa Hama katika kipindi cha wiki moja iliopita.

Waasi katika jimbo la Hama nchini Syria.
Waasi katika jimbo la Hama nchini Syria.Picha: Reuters/A. Abdullah

Maeneo yanayoshambuliwa kwenye viunga vya kaskazini vya mji wa Homs yanadhibitiwa na waasi wa Kiislamu wa itikadi kali likiwemo tawi la Al Qaeda la al- Nusra Front ambao wanapambana na vikosi vya Assad halikadhalika wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu.

Mashambulizi hayo ya ardhini na anga katika mji wa Homs yanakuja wakati kukiwa na repoti kwamba maelfu ya wapiganaji wa Iran wamewasili Syria kuvisaidia vikosi vya Assad.

Putin ashutumu Marekani

Alhamisi Rais Vladimir Putin wa Urusi ameshutumu msimamo wa Marekani kwa Syria kuwa sio wa tija baada ya Marekani kukataa kuupokea ujumbe wa Urusi huko Washington unaoongozwa na Waziri Mkuu Dmitry Medvedev.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: AFP/Getty Images/A. Nikolsky

Putin amekaririwa akisema "Naamini kwamba msimamo huu hauna tija.Sifahamu vipi washirika wetu wa Marekani wanaweza kuishutumu hatua za Urusi kupambana na ugaidi nchini Syria wakati wakikataa kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja juu ya suala muhimu kabisa la usulihishi wa kisiasa."

Akizungumza katika kikao cha bunge la Ujerumani Alhamisi Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameitaka Urusi iwe sehemu ya kutafuta usuluhishi wa kisiasa nchini Syria.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa/afp

Mhariri :Yusuf Saumu