1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaipiku Marekani kuifadhili Yemen kwa silaha

Kabogo Grace Patricia6 Januari 2010

Inadaiwa kuwa Urusi na China zimekuwa zikitoa silaha zenye thamani ya mamilioni ya dola kusaidia vikosi vya jeshi la Yemen.

https://p.dw.com/p/LMWL
Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen.Picha: picture-alliance/ dpa

Urusi imeipiku Marekani katika soko la silaha la thamani ya mamilioni ya dola nchini Yemen, ambayo ununuzi wake wa silaha, kwa sehemu kubwa, unafadhiliwa na nchi jirani ya Saudi Arabia. Vikosi vya jeshi vya Yemen ambavyo vimekuwa vikijirekebisha kuendana na wakati wa sasa juu ya mpango wa kijeshi wenye kugharimu dola zinazokisiwa kufikia bilioni nne, vina silaha ambavyo, kwa sehemu kubwa, zinatokea Urusi, China, Ukraine, Ulaya Mashariki na jamhuri za zamani za Kisovieti. Pamoja na jaribio la shambulio la kutaka kuiripua ndege ya abiria ya Marekani siku ya Krismasi lililofanywa na mwanafunzi, raia wa Nigeria, anayeripotiwa kupatiwa mafunzo na kundi la al-Qaeda nchini Yemen, utawala wa Rais Barack Obama umeahidi kuongeza mara mbili jeshi lake na kutoa msaada wa karibu dola milioni 150 kwa ajili ya kupambana na ugaidi ili kuiimarisha zaidi serikali ya Rais Ali Abdullah Saleh.

Thamani ya silaha ambazo Yemen inapokea

Kwa sasa Yemen inapokea msaada kutoka kwa miradi inayofadhiliwa na Marekani, ikiwemo ya ufadhili wa jeshi la nje-FMF, mafunzo na utoaji elimu kwa jeshi la kimataifa-IMET, kuzuia uenezaji wa silaha, kupinga ugaidi pamoja na kupambana na silaha za maangamizi. Lakini mapendekezo ya misaada ya kijeshi ya Yemen pamoja na usambazaji wa silaha za Marekani yanaonekana kutokuwa muhimu au sawa na bure, ukilinganisha na msaada wa silaha, mafunzo ya kijeshi na utaalamu wa kiufundi unaotolewa na vyanzo ambavyo si vya ki-Marekani. Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm-SIPRI, kuanzia mwaka 2004 hadi 2008, Urusi imeipatia Yemen karibu asilimia 59 ya silaha kubwa, ikifuatiwa na Ukraine iliyoipa silaha kwa asilimia 25, Italia ilitoa asilimia 10, Australia asilimia 5 na Marekani chini ya asilimia moja.

Yemen yasaini mpango wa kununua silaha Urusi

Mkurugenzi wa mpango wa kuhamisha silaha wa SIPRI, Dokta Paul Holtom, ameliambia shirika la habari la IPS kuwa vyombo vya habari vya Urusi vilitangaza kuwa mwanzoni mwa mwaka huu Yemen imesaini mpango wa kununua silaha zinazokadiriwa kufikia dola bilioni moja kutoka Urusi. Kwa mujibu wa Idara ya Utafiti ya CRS, kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, Yemen ilipokea silaha zenye thamani ya dola bilioni 1.4, katika hizo silaha za thamani ya dola milioni 600 zilitoka Urusi. China ilitoa silaha zenye thamani ya dola milioni 200, huku silaha nyingine za thamani ya dola milioni 400 zikitoka katika jamhuri za zamani za Kisovieti na mataifa ya Ulaya Mashariki, hasa Ukraine, lakini pia Belarus, Jamhuri ya Cheki, Poland, Italia na nyinginezo. Pamoja na vitisho vipya vya kigaidi kutoka kwa wanamgambo wa Yemen, Marekani inajidhatiti zaidi katika kuimarisha njia zake mpya za kupambana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, mbali na njia zinazotumika sasa nchini Iraq, Afghanistan na Somalia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)

Mpitiaji: Othman Miraji