1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yajiimarisha kijeshi mpakani mwa Ukraine

Mohammed Abdul-Rahman 5 Novemba 2014

Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema majeshi ya Urusi yameonekana yakisongea kuelekea mpaka wa Ukraine na kuitaka Urusi ichukuwe hatua za dhati kuutatua mgogoro wa Mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1DgyC
Magari ya kivita ya Ukraine
Magari ya kivita ya UkrainePicha: AFP/Getty Images

Katibu mkuu wa NATO Stoltenberg alisema mjini Brussels kwamba Urusi inaendelea kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine kwa kuwapa zana na kutuma kikosi chake maalum ndani ya Ukraine.

Taarifa hiyo ya harakati mpya za Urusi nchini Ukraine, inakuja siku moja baada ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuondoa uwezekano wa kuchukuliwa hatua yoyote ili kumaliza vikwazo vya kimataifa dhidi ya Ukraine kutokana na hali ya wasi wasi inayoendelea.

Merkel alikuwa akizungumza na viongozi wa kibiashara na akaitaka Urusi itumie ushawishi wake kwa wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine ili watekeleze makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliofikiwa mjini Minsk, Jamhuri ya Belaruss.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Reuters/Francois Lenoir

Huko Ukraine kwenyewe serikali imelaani kuapishwa viongozi wawili wa maeneo yanayotaka kujitenga-Jamhuri ya Donetsk na Jamhuri ya watu wa Luhansk, baada ya uchaguzi wa Jumapili katika maeneo hayo na ambao hautambuliwi si na Ukraine wala Jumuiya ya kimataifa , ukiwemo Umoja wa Ulaya.

Mapema leo viongozi wa wanaotaka kujitenga waliwashutumu maafisa wa Ukraine wakidai kuwa ni wao wenye kuhujumu hatua ya kupata amani baada ya kusitisha sheria inayotoa madaraka maalum kwa mikoa ya mashariki.

Wanajeshi wa Ukraine kupelekwa maeneo ya Mashariki kwa ulinzi zaidi

Wakati Urusi ikisemekana kujiimarisha kijeshi katika mpaka na Ukraine, Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema Ukraine inatuma vikosi kuilinda miji mashariki mwa nchi hiyo dhidi ya jaribio la waasi kutwaa maeneo zaidi.

Akizungumza katika mkutano wa wakuu wa idara za usalama mjini Kiev Poroshenko alisema jeshi liko tayari kulizima jaribio lolote la mashambulizi ya waasi, lakini pamoja na hayo bado hajayaweka kando makubaliano yaliofikiwa mwezi Septemba, kumaliza mgogoro huo.

Kwa upande mwengine kuliripotiwa mapigano mapya katika eneo hilo la mzozo ambapo mwanajeshi mmoja wa serikali aliuwawa na watano kujeruhiwa. Mkuu mpya wa sera ya kigeni wa Umoja wa ulaya Federica Mogherini kuna hatari ya kufuja nafasi ya mazungumzo ya ndani Ukraine na pia pamoja na Urusi, kumaliza mgogoro huo.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: picture-alliance/dpa/ ITAR-TASS/Palinchak

Mgogoro wa Ukraine umesababisha mvutano mkubwa katika uhusiano baina ya Urusi na nchi za magharibi, usiowahi kuonekana tokea kumalizika kwa vita baridi kati ya mashariki na magharibi., kufuatia kuanguka kwa Ukoministi.

Mjini Moscow, msemaji wa Ikulu Dimitri Pestov amesema hakuna mazungumzo yaliopangwa kati ya rais Barack obama wa Marekani na Vladimir Putin wa Urusi watakapokuwa katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya mataifa ya Asia na Pacific mjini Beijing Jumatatu na Jumanne ijayo na ule wa nchi za kundi la G20 utakaofanyika nchini Australia tarehe 15 na 16 ya mwezi huu wa Novemba.

Mwandishi : Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri:Josephat Charo