1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yalipiza kisasi dhidi ya Marekani

John Juma
28 Julai 2017

Urusi imeiamuru Marekani kupunguza idadi ya wanadiplomasia na maafisa wake wengine walioko katika ubalozi wa Moscow hadi wabakie 455 pekee ifikapo tarehe mosi Septemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/2hKRe
Moskau US Botschaft Gebäude
Picha: Getty Images/AFP/K. Kudryavtsev

Urusi imeiamuru Marekani kupunguza idadi ya wanadiplomasia na maafisa wake wengine walioko katika ubalozi wa Moscow. Kadhalika Urusi imeuzuia ubalozi huo kutumia jengo la Moscow la mikutano na la maghala. Hatua hiyo ni ya kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya mapendekezo mapya ya Marekani kuiwekea Urusi vikwazo vipya.

Tangazo hilo limetolewa leo na wizara ya mambo ya nje ya Urusi. Wizara hiyo imeitaka Marekani kupunguza idadi ya wanadiplomasia wake pamoja na maafisa wake wengine hadi wabakie 455 pekee ifikapo tarehe mosi Septemba mwaka huu. Aidha itachukua baadhi ya vitu vya kidiplomasia vya ubalozi huo.

Wizara hiyo imesema kuwa hatua hiyo imesababishwa na hatua mpya ya bunge la seneti la Marekani kupitisha mswada wa kuiwekea Urusi vikwazo vipya.

Changamoto kwa Trump

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/Newscom/C. Kleponis

Mswada huo uliopitishwa kwa pamoja na wabunge wa Republican na Democrat, unamweka Rais Donald Trump katika hali ngumu ya kuuidhinisha hivyo kuiwekea Urusi masharti magumu au kuukataa hali itakayomweka katika njia panda na wanachama wake wa Republican. Kwa mujibu wa ripoti katika shirika la habari la RIA, ambayo ilinukuu vyanzo vya habari, Marekani itapunguza kati ya maafisa wake 200-300 katika ubalozi huo.

Moscow ilisema kuwa mswada huo mpya unaonesha kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na Marekani umefungwa kwenye makabiliano ya kisiasa ndani ya Marekani. Ilionya kuwa ina haki ya kuchukua hatua nyinginezo zinazoweza kuathiri Marekani.

Kadhalika rais wa Urusi Vladimir Putin hapo jana alikashifu kile alichokiita kuwa Marekani kueneza hofu dhidi ya Urusi, jambo ambalo Urusi haiwezi kuendelea kukubali. Putin alielezea masikitiko yake kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Urusi. "Bila shaka tunasikitishwa. Tunasikitishwa kwa sababu lau tungefanya kazi pamoja tungesuluhisha mambo mengi vyema na  masuala muhimu ya msingi yanayohusu Warusi na Wamarekani."

Balozi wa Marekani nchini Urusi, John Tefft ameelezea kusikitishwa na tangazo hilo la Moscow. Hata hivyo msemaji wa ubalozi huo alikataa kuelezea idadi kamili ya maafisa walioko Moscow.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Martin Schaefer
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Martin SchaeferPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Ujerumani yaonya Marekani dhidi ya vikwazo hivyo

Wakati huohuo, Ujerumani imeionya Marekani kuwa haitakubali vikwazo dhidi ya Urusi ambavyo pia vinalenga kampuni za Ulaya. Japo amesisitiza umuhimu wa kuongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Urusi kuhusu wajibu wake kwenye mzozo wa Ukraine, waziri wa mambo ya nje Simar Gabriel amesema sera ya kutumia vikwazo si suluhisho muafaka kuhusu masilahi ya uuzaji wa kitaifa na kuhusu sekta ya nishati.

Martin Schaefer ambaye ni msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani anaeleza. "Nimejaribu kufafanua hilo kwamba kwa ujumla hatuwezi kukubali kuwa serikali ya Marekani, siasa za Marekani, bunge la Marekani kutumia vikwazo kama kisingizio kuweka sera zitakazopendelea makampuni ya Marekani ya kusambaza nishati."

Mataifa ya Ulaya yameishutumu Washington kuhusu athari za vikwazo vipya, yakisema yataathiri kampuni zao zinazohusika katika ujenzi wa bomba jipya la gesi kutoka Urusi kupitia bahari ya Baltic kuelekea Ujerumani. Umoja wa Ulaya pia imeonya kuwa itachukua hatua za haraka za kulipiza kisasi endapo Marekani haitatilia maanani wasiwasi wao.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo