1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yalitaka Baraza la Usalama kuichukulia hatua Syria

16 Desemba 2011

Urusi imekabidhi rasimu mpya juu ya ghasia za Syria kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutoa matumaini ya hatua kali kufuatia kuuwawa kwa askari 27 wa Syria na kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/13U39
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly ChurkinPicha: AP

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amewaambia waandishi wa habari kuwa rasimu mpya ya taifa hilo juu ya ghasia za Syria imeipa nguvu rasimu ya mwanzo na imeweka wazi kuwa wakuu wa Syria wanahusika pakubwa katika kukandamiza wa haki za binadamu.

Churkin anasema Urusi imewasilisha rasimu hiyo mpya kwa baraza hilo na tumependekeza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya Syria kufuatia vitendo vya ukandamizaji wa haki za binadamu na kuhakikisha wanaacha mara moja machafuko na kuharakisha kufanya mabadiliko.

Rasimu hiyo mpya ya Urusi haikuamini iwapo pande zote mbili za Syria zilihusika katika machafuko, lakini ilizitaka pande hizo ziache mara moja vitendo hivyo na rasimu hiyo haikuwa na tishio lolote la vikwazo, jambo ambalo Moscow iliendela kulipinga.

Maofisa wa mataifa ya magharibi wamefurahishwa na hatua hiyo ya Urusi, lakini Balozi wa Ufaransa, Gerrad Araud, ameibuka na kusema rasimu hiyo inahitaji marekebisho makubwa zaidi ya hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary ClintonPicha: dapd

Kwa upande wa Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton hajaunga mkono baadhi ya vipengele vya rasimu hiyo mpya, lakini akaahidi kufanya kazi pamoja na serikali ya Dmitry Medvedev katika hilo.

Bi. Clinton ameipongeza pia Urusi kwani ni mara ya kwanza kutambua kuwa suala la mgogoro wa kisiasa nchini Syria linastahili kufikishwa katika Baraza la Usalama la UN.

Akiwa jijini London, Uingereza, waziri katika Ofisi ya Mambo ya Nje, Alistair Burt, anaona Urusi ina nafasi muhimu katika kuweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya serikali ya Bashaar al- Assad.

Aidha, Burt amesema Uingereza itajaribu kutafuta njia nyingine mbadala za kuamuru vikwazo vipya kwa Damascus, kufuatia utumiaji wa nguvu kubwa kwa waandamanaji.

Kupitia Umoja wa Ulaya, Burt amesema London itaiwekea Syria vikwazo katika sekta za kifedha, nishati na usafiri ili kuuadhibu utawala wa nchi hiyo ya kiarabu.

Katika ripoti yake ya jana, Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, baada ya kuwahoji waasi wa serikali hiyo, linasema makamanda wa jeshi waliamuru vikosi vya serikali kutumia njia yoyote iwezekanayo kuyazima maandamano na aghalabu kutoa maelekezo kamilifu ya kuwafyatulia risasi raia wasio na hatia.

Shirika hilo limewatambua makamanda sabini na nne waliotoa kibali cha kuua, kutesa na kuwakamata watu kinyume cha sheria na imesema bayana kuwa huo ni uhalifu dhidi ya binaadamu, na hivyo kuliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuishtaki Syria mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC.

Mwandishi: Pendo Paul/Reuters

Mhariri: Miraji Othman