1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAAF yaipiga marufuku Urusi kwa muda

14 Novemba 2015

Shirikisho la riadha la Urusi limefungiwa kwa muda kushiriki katika mashindano ya kimataifa, ikiwemo michezo ya Olimpiki, kwa tuhuma za kuhusika katika matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini

https://p.dw.com/p/1H5vq
Weltverband IAAF Leichtathletik Doping Skandal Russland
Picha: picture-alliance/dpa/H. Hanschke

IAAF imechukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa kwa ripoti ya shirika la kimataifa la kukabiliana na dawa zilizopigwa marufuku michezoni - WADA iliyodai Urusi imekuwa “ikisaidia katika matumizi ya dawa za kuongeza nguvu misuli”.

Wanachama wa baraza la shirikisho hilo la riadha duniani walipiga kura 22-1 kuunga mkono Urusi ipigwe marufuku.

“Huu ni ujumbe muhimu sana kwetu,” amesema rais wa IAAF Sebastian Coe, akiongeza kuwa amejitolea kufanikisha mabadiliko. Amesema tunahitaji kujitafakari upya, kujichunguza sisi wenyewe katika mchezo huu, na tutafanya hilo.” Naye waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko amesema marufuku hiyo ni ya “muda” na ni “tatizo linaloweza kutatuliwa”.

Mwakilishi wa taifa hilo katika baraza la IAAF hakuruhusiwa kushiriki kwenye kura hiyo iliyopigwa Ijumaa. Jinsi mambo yalivyo kwa sasa, wanariadha wa Urusi hawawezi kushiriki mashindano ya kimataifa ya riadha, ikiwemo msururu wa mashindano ya riadha duniani na michezo ya Olimpiki ya Rio itakayoanza Agosti mwaka ujao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo