1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yarefushiwa vikwazo vya kiuchumi

Admin.WagnerD22 Desemba 2015

Umoja wa Ulaya umerefusha muda wa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi kutokana na nchi hiyo kushindwa kutekeleza mkataba wa amani. Umoja huwo pia unailaumu Urusi kwa kushindikana kwa mazungumzo ya biashara baina yao

https://p.dw.com/p/1HRaN
Russland Jahrespressekonferenz Präsident Wladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/M. Zmeyev

Urusi imesema uamuzi huo unaonesha kuwa Umoja wa Ulaya hauna dhamira ya kuimarisha mahusiano na nchi hiyo, ili kuweza kupambana na vitisho vinavyoikabili dunia kama vile ugaidi.

Wakati huohuo Umoja wa Ulaya pia unailaumu Urusi kwa kushindikana kupatikana makubaliano katika mazungumzo ya mwisho yanayolenga kupunguza wasiwasi wa Urusi juu ya mkataba wao na Ukraine wa biashara huria unaotegemewa kuanza rasmi Januari mosi.

"Tulidhani kwamba kuna umuhimu wa kuwa na mkutano huu leo, ili kuona kama kuna utayari wa kutafuta njia za makubaliano, kwa bahati mbaya haikuwa hivyo. Tumetumia siku nzima kujaribu kujadili lakini hapakuwa na makubaliano hivyo zoezi hili sasa limemalizika," amesema Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmstroem.

Urusi inadai makubaliano hayo ya biashara baina ya Umoja wa Ulaya na Ukraine yatadhoofisha maslahi yake nchini Ukraine na yataruhusu biashara za bei nafuu kumiminika ndani ya nchi hiyo ikiwa ni moja wapo ya masoko yake muhimu ya biashara.

Vikwazo dhidi ya Urusi

Cecilia Malmström PK 04.12.2013
Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia MalmstroemPicha: Georges Gobet/AFP/Getty Images

Aidha kuhusu vikwazo dhidi ya Urusi, wizara ya wa mambo ya nje ya Urusi imesema katika taarifa yake kwamba, badala ya kujenga mahusiano mazuri baina yao ili kuweza kupambana na changamoto kadhaa zinazoikabili dunia kwa sasa, kama vile ugaidi wa kimataifa, Umoja wa Ulaya badala yake umeamua kuendelea na mchezo wake wa malemgo mafupi wa kuiwekea Urusi vikwazo.

Baraza la Umoja wa Ulaya lenye nchi wanachama 28 wamekubaliana kurefusha vikwazo hivyo vya kiuchumi kwasababu mkataba wa amani-- uliofikiwa baina ya Ufaransa, Ujerumani, Ukraine na Urusi katika mazungumzo yaliyofanyika katika mji mkuu wa Belarus, Minsk -- hautowezekana kutekelezwa kikamilifi ifikapo mwisho wa mwaka kama walivyokubaliana awali.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo la Umoja wa Ulaya imesema, kwavile makubaliano ya Minsk yatashindwa kutekelezwa kikamilifu ifikapo Disemba 31 mwaka huu, muda wa vikwazo dhidi ya Urusi umerefushwa huku baraza hilo likiendelea kutathmini maendeleo ya utekelezaji.

Umoja wa Ulaya kwa mara ya kwanza uliiwekea Urusi vikwazo kwa muda wa mwaka mzima baada ya kuangushwa kwa ndege ya shirika la ndege la Malaysia Airlines, kitendo kilicholaumiwa wanamgambo wa mashariki mwa Ukraine wanaoegemea upande wa Urusi. Na mnamo Juni mwaka huu, vikwazo vilirejeshwa upya kwa miezi mengine sita hadi Januari ya mwaka 2016 na kwa sasa vikwazo hivyo vitarefushwa hadi mwisho wa mwezi Julai ya mwaka 2016.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp

Mhariri: Yusuf Saumu