1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urussi na Marekani zalumbana tena juu ya mpango wa makombora ya Ulinzi

9 Julai 2008

Urussi yasema italazimika kutumia nguvu za kijeshi ikiwa Marekani itaandelea na mpango wa kuweka makombora ya ulinzi karibu na nchi yake.

https://p.dw.com/p/EYuM
Ndege za kijeshi za UrussiPicha: AP

Urussi imetoa kitisho hicho kikali dhidi ya mpango wa Marekani wa kutaka kuweka makombora ya ulinzi karibu na nchi yake muda mfupi baada ya waziri wa mambo ya nje Condolezza Rice kusaini makubaliano ya mwanzo na Jamhuri ya Czech ambayo ni sehemu ya mpango huo wa Marekani.Makubaliano hayo yataifungulia njia Marekani kuweka mtambo wake radar katika ardhi ya Jamhuri ya Czech.

Marekani imeyaita matamshi ya Urussi kuwa ya ugomvi yanayolenga hasa kuwatia uoga washirika wake wa kimkakati barani ulaya kuhusiana na mpango wake huo .

Balozi wa Urussi katika Umoja wa mataifa Vitaly Churkin amesema '' Kila hatua ya kijeshi inajibiwa kijeshi.Hii ni sheria ya kimsingi katika jeshi.Ikiwa kunatokea hatua ya kijeshi au kuna mabadiliko ya msimamo wa kimkakati,basi inabidi kuweko hatua za kuchukuliwa kukabiliana na hali hiyo.Hii imebainishwa wazi katika kila kitabu cha sheria za kijeshi,kwahivyo hakuna la ajabu hapo na wala hakuna suali la kuulizwa''

Aidha wizara ya mambo ya nje ya Urussi imetoa taarifa ya kusisitiza kwamba haitochukua hatua za kidiplomasia punde Marekani itatimiza lengo lake hilo.

Urussi inasema kuweka mfumo wa makombora ya ulinzi karibu na mipaka yake itadhoofisha ulinzi wake.Mwanzoni nchi hiyo ilitishia kuweka makombora yake ya kujilinda katika kambi yoyote ya mpango huo wa Marekani iwe ni Poland au Jamhuri ya Czech.

Urussi pia imesema itaendelea kufuatilia hali ya mambo na pia inabakisha milango yake wazi kwa ajili ya mazungumzo ya dhati juu ya suala hilo la mkakati wa kiusalama.

Lakini Marekani inasema Urussi inabidi kutambua kwamba ni muhimu kuwa washirika sawa na Marekani katika mpango huo wa ulinzi.

Marekani inadai kuwa moango huo ni muhimu katika kuzuia uwezekano wa mashambulio ya kile inachoziita ni mataifa wachokozi kama vile Iran ambayo ni adui wake mkubwa. Waziri wa mambo ya nje Condolezza Rice anasema'' Tumeshaileza Urussi kwamba sote tunakabiliwa na kitisho kutoka mataifa kama Iran ambayo yanaendelea kutengeneza makombora ya masafa marefu na ni lazima tuwe katika nafasi ya kuweza kujibu''.

Hata hivyo kwa upande mwingine raia wengi wa Jamhuri ya Czech wanaupinga vikali mpango huo,maelfu waliandamana jana na kuishutumu hatua ya serikali yao ya kuunga mkono.

Lakini mpango huo haujapita moja kwa moja kwani sasa utabidi upitishwe bungeni ambapo itategemea ikiwa upinzani utaupigia kura.

Marekani hadi sasa imeshindwa kuishawishi Poland kutia saini makubaliano kama hayo.