Usain Bolt awaaga mashabiki wake
14 Agosti 2017Wiki hii mashabiki katika michezo ya ubingwa wa dunia walishuhudia mkimbiaji maarufu Usain Bolt akiwaaga mashabiki , lakini kwa masikitiko makubwa wakati aliposhindwa kuanga kwa kung'ara , baada ya kuambulia medali ya shaba tu katika mbio zake maarufu za mika 100 na pia kushindwa kabisa kuambulia kitu katika mbio za mita 400 kupokezaja vijiti.
Zaidi ya mashabiki 700,000 walijitokeza katika uwanja wa Olimpiki katika kipindi cha michezo hiyo ikiwa ni rekodi ya juu kabisa , na kuupa mchezo huo nguvu inayohitajika baada ya baadhi kudokeza kwamba Bolt pekee ameiweka michezo ya riadha katika mwanga katika muda wa miaka iliyopita kwa kasi yake na muonekano wake. Katika mkutano na waandishi habari Bolt alisema.
"Kwangu mimi ilikuwa safi kabisa, unafahamu nini ninachomaanisha. Uungwaji mkono haujabadilika, unafahamu ninachomaanisha. Nilitarajia hilo. Inasikitisha kwamba inabidi niondoke hivi sasa. Lakini hamasa ya mashabiki ilikuwa ya hali ya juu kabisa kama kawaida na nimewapenda , wamenifanya nijisikie niko nyumbani na kuwa nakaribishwa. Wapenzi wangu kwa kweli wananipenda na naikubali sana hali hiyo."
Karibu atoke mikono mitupu
Bolt aliingia mjini London kwa ajili ya mashindano haya akiwa na mataji 11 ya ubingwa wa dunia na dhahabu 8 za olimpiki lakini aliondoka karibu mikono mitupu. Alinyakua shaba tu katika mbio za mita 100 na kupata maumivu ya paja katika mita 400 kupokezana vijiti. Na ameahidi kwamba hatarejea tena uwanjani kama mwanariadha na hajutii kwamba hakustaafu mwaka jana baada ya kupata medali tatu za dhahabu mjini Rio.
"Kwangu mimi nilikuwa nasema kwaheri kwa mashabiki wangu na nasema tu kwaheri kwa mbio ninazoshiriki. Hizi ni mbio zangu mbili ambazo nilidhibiti kwa miaka kadhaa , kwa hiyo nilikuwa nasema kwaheri kwa kila kitu, mnafahamu kile ninachomaanisha. Nafikiri karibu niangue kilio. Ilikuwa karibu lakini haikufikia hivyo nilikuwa naaga. Hivyo ndivyo ilivyokuwa , nilikuwa naaga matukio ya michezo yangu."
Mbali na Bolt , Mo Farah wa Uingereza pia alikosa kukamilisha fainali yake muhumu baada ya kushindwa mbio za mita 5,000 na kuambulia medali ya fedha licha ya kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 10,000.
Caster Semenya wa Afrika kusini alinyakua medai ya dhahabu katika mbio za 800 wanawake , na hapo kabla alishinda mbio za mita 1,500.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /dpae / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef