1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama kuimarishwa wakati wa michezo ya Olimpiki

Charo, Josephat24 Machi 2008

Mwenge wa Olimpiki kuwashwa leo mjini Olympia Ugiriki

https://p.dw.com/p/DTST
Kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai LamaPicha: AP

China imesema itaimarisha usalama wakati mwenge wa michezo ya Olimpiki utakapokuwa ukipitia Tibet kwenda mlima Everest, huku serikali ikijaribu kuzuia maandamano ya kuvuruga juhudi za kudhihirisha umoja wa kitaifa. Kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama ameshutumiwa kuwa na njama ya kuyavuruga mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu mjini Beijing China.

China leo imeimarisha usalama katika maeneo yanayokabiliwa na machafuko yanayopakana na Tibet, huku maafisa wengi wa usalama wakiwazuia waandishi wa habari wa kigeni wasiingie katika maeneo yanayokaliwa na Watibet wengi. Madereva wa teksi katika eneo hilo wamesema wameamriwa na polisi na wanajeshi wasitoke mji wa Kangding kwenda katika eneo la magharibi la mji huo.

China imeongeza juhudi za kutaka kuugwa mkono wakati wa michezo ya Olimpiki mjini Beijing huku jumuiya ya mataifa ikiukodolea macho mzozo wa Tibet. Serikali ya mjini Beijing inamlaumu kiongozi wa dini ya kibudha Dalai Lama kwa machafuko ya Tibet.

Shirika la habari la Xinhua nchini China limeripoti hii leo kwamba matamshi ya Dalai Lama ya kuunga mkono michezo ya Olimpiki yamedhihirika kuwa ya uongo kwa kuwa wafuasi wake wameugomea mwenge wa michezo hiyo na kufanya machafuko mjini Lhasa na kwingineko. Ripoti hiyo imesema njama ya kuihujumu michezo ya Olimpiki haitafaulu.

China inadai Dalai Lama alipanga kuyavuruga mashindano ya Olimpiki kwa kuandaa maandamano yaliyoanza kwa mikutano ya amni ya hadhara katika mji mkuu wa Tibet, Lhasa mnamo tarehe 10 mwezi huu, kuadhimisha miaka 49 ya mapinduzi dhidi ya utawala wa China yaliyoshindwa. Siku tano baadaye maandamano hayo ya amani yaligeuka kuwa ya machafuko na kuenea katika maeneo mengine ya Tibet.

Dalai Lama amekanusha madai ya China kwamba amehusika kupanga machafuko ya Tibet na kusema haipingi michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Beijing.

Afisa wa ngazi ya juu wa China aliyehukumiwa kifungo gerezani kwa maandamano katika uwanja wa Tiananmen, Bao Tong, ameitolea mwito China ifanye mazungumzo na Dalai Lama, ili kuumaliza mgogoro wa Tibet.

Pelosi akosolewa

China imemueleza spika wa bunge la Marekani, Nacy Pelosi, kuwa mlinzi wa wahalifu, majambazi na wauaji, baada ya kumtembelea Dalai Lama huko Dharamshala nchini India, na kuishutumu serikali ya Beijing kwa ukandamaziji huko Tibet. Katika taarifa iliyochapishwa leo, China imesema bi Nancy Pelosi alipoteza mamlaka yake kuweza kuzungumzia haki za binadamu.

Taarifa hiyo pia imesema wakitafuta sababu za kuichafulia jina China, polisi wanaolinda haki za binadamu kama vile Pelosi, wana hasira na hawana ukarimu wanapoishughulikia China. Hukataa kuchunguza matamshi yao na kutafuta ukweli wa mambo.

Maandamano

Wakati haya yakiarifiwa, polisi nchini Nepal wamewatawanya wakimbizi na watawa wa kibudha 200 wa Tibet waliokuwa wakiandamana karibu na ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Kathmandu hii leo. Polisi wamewatandika waandamanaji hao kutumia fimbo za mianzi na kuwatia mbaroni watu 40. Waandamanaji hao wanautaka Umoja wa Mataifa uchunguze ukandamaziji wa maandano ya Tibet uliofanywa na maafisa wa China.

Wakipiga kelele za kuitaka China ikomeshe mauaji ya Watibet, waandamanji hao walitembea kwenda katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Kathmandu wakati polisi walipowasimamisha yapata mita 100 kabla kuyafikia makao hayo na kuwapokonya mabango waliyokuwa wameyabeba.

Mwenge

Na habari za hivi punde zinasema rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki, Jacques Rogge, amesema leo mjini Olympia nchini Ugiriki kwamba haoni dalili za uungwaji mkono wa kimataifa kuyagomea mashindano ya Olimpiki mjini Beijing kwa hatua ya China kuyakandamiza maandamano ya Tibet.

Akihudhuria sherehe ya kuuwasha mwenge wa michezo hiyo kiongozi huyo amesema uamuzi wa kuipa fursa China kuandaa michezo hiyo ulikuwa sawa, licha ya kuwa na rekodi mbaya kuhusu haki za binadamu.