1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alama za vidole zagunduliwa

Admin.WagnerD8 Januari 2016

Maafisa waliokuwa wanafanya uchunguzi katika nyumba moja mjini Brussels wamegundua alama za vidole za gaidi alieshiriki katika mashambulio yaliyofanyika mjini Paris mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/1HaOG
Polisi walinda usalama baada ya mashambulio ya kigaidi mjini Paris
Polisi walinda usalama baada ya mashambulio ya kigaidi mjini ParisPicha: Reuters/C. Platiau

Mwendesha mashtaka wa serikali, pia amethibitisha kugunduliwa kwa alama za mikanda ya kujitolea mhanga iliyotumika katika mashambulio hayo.

Taarifa imesema makaazi yaliyopo katika ghorofa ya tatu ,ya nyumba hiyo,iliyoko katika kitongoji cha Schaerbeek cha mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels ilipekuliwa tarehe 10 mwezi Desemba.

Aliyekodi makaazi hayo alitoa taarifa bandia ambazo yumkini zilitumiwa na mmojawapo wa watu 10 waliokamatwa nchini Ubelgiji kutokana na kutuhumiwa kuhusika na mashambulio ya mjini Paris ambapo watu 130 waliuliwa mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, alama za vidole zilizogunduliwa ni zile za Salah Abdeslam ambae mpaka sasa bado anatafutwa .

Mwendesha mashtaka mkuu nchini Ubelgiji Eric Van Sypt amesema ,katika makaazi hayo ,yaliyopekuliwa, wachunguzi pia waligundua nyenzo zinazoweza kutumika kwa ajili ya kutengenezea mabomu. Inaaminika kwamba Abdelslam ndiye aliekuwa na dhima kubwa zaidi katika maandalizi ya mkakati wa mashambulio ya mjini Paris.

Habari zinasema polisi wa Ufaransa walimsimamisha gaidi huyo pamoja na rafiki zake wawili waliokuwamo ndani ya gari, karibu na mpakani lakini baadae waliachiwa wapite.

Maafisa wa idara ya usalama wanaamini kwamba Abdelslam alirejea kwenye makaazi ya kitongoji cha Schaarbeek ambapo alichukuliwa na mtu mwengine, na tangu wakati huo hajaonekana tena.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Ubelgiji Eric Van Sypt amesema anaamini magaidi walikuwa wanayatumia makaazi hayo ili kujificha. Nyumba hiyo ya magaidi ilisachiwa mnamo mwezi wa Desemba lakini taarifa imetolewa baada ya mwezi mmoja. Hakuna maelezo yaliyotolewa , juu ya kuchelewa kuitoa taarifa hiyo.

Polisi wafanya msako wa magaidi mjini Brussels
Polisi wafanya msako wa magaidi mjini BrusselsPicha: picture-alliance/dpa/N.Maeterlinck

Magaidi wanaoitwa dola la kiislamu walidai kuhusika na mashambulio yaliyofanyika kwenye mikahawa na sehemu nyingine za burudani katika mji wa Paris. Magaidi saba pia walikufa, lakini idadi kamili ya walioshiriki katika mauaji haijajulikana kwa uhakika.

Lakini ni hakika kwamba miongoni mwa magaidi waliokufa alikuwa ndugu yake Abdeslam. Idara za usalama za Ubelgiji zimesema miongoni ,wa watu 10 waliokamatwa kuhusiana na mauaji ya mjini Paris walikuwamo wale waliomsaidia Abdelslam.

Urafansa ilishasema muda mrefu kwamba mauaji ya mjini Paris yalipangwa na magaidi nchini Ubelgiji na kwamba kiongozi wa mikakati alikuwa Abdelhamid Abaaoud aliekuwa mkaazi wa mjini Brussels. Gaidi huyo aliuliwa na polisi wakati wa msako uliofanywa mjini Paris baada ya mashambulio ya magaidi.

Mwandishi;Mtullya Abdu.afpe/

Mhariri: Iddi Ssessanga