1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi kwa Wataliban?

Maja Dreyer30 Agosti 2007

Suala moja linalozungumziwa ni kisa cha mateka wa Korea Kusini ambao saba bado wako mikononi mwa Wataliban, lakini wanatarajiwa kuachiliwa leo.

https://p.dw.com/p/CHRy

Juu ya kesi hiyo na matokeo yake, mhariri wa “Leipziger Volkszeitung” ameandika:

“Kwa mara ya kwanza serikali iliyotuma majeshi nchini Afghanistan ilizungumza ana kwa ana na Wataliban. Hiyo itawatia moyo wahalifu na wanamgambo wengine kufanya vivyo hivyo, yaani kuwateka nyara wageni. Kwa upande wa nchi za kigeni itakuwa vigumu zaidi kutoyakubali matakwa ya watekaji nyara. Yule ambaye anaikosoa serikali ya Korea Kusini kwamba kwa kukubali matakwa ya Wataliban inalipa nguvu kundi hilo ambalo liliwahi kuitawala Afghanistan, basi mtu huyu hafahamu hali halisi. Kwanza, wanamgambo hao wanaofuata itikadi kali za Kiislamu tayari wamepata nguvu. Na pili: kesi za utekaji nyara si chanzo cha shida ilioko nchini Afghanistan, bali ni ishara kwamba mkakati wa jumuiya ya kimataifa kuleta amani Afghanistan umeshindwa.”

Ni uchambuzi wa mhariri wa “Leipziger Volkszeitung”. Mwingine tunasoma katika “Allgemeine Zeitung” la mjini Mainz:

“Mateka wa Korea Kusini wameachiliwa huru na wanaweza kurudi makwao wakiwa bado hai. Hizi ndizo habari nzuri kutoka Afghanistan. Habari mbaya lakini zinazidi. Kesi hiyo ya Wakorea Kusini kwa mara nyingine imeonyesha kwamba vitendo vya utekaji nyara vinaleta faida kwa wahalifu. Haya yalikuwa wazi hata kabla ya Korea Kusini kukubaliana na Wataliban, lakini sasa yamehakikishwa. Kwa hivyo, Kwa wageni wanaofanya kazi Afghanistan maisha yanazidi kuwa hatarini.”

Katika gazeti la “Neue Ruhr” tunasoma ukosoaji mkali dhidi ya serikali ya Korea Kusini na namna ilivyoitatua kesi hiyo:

“Bila shaka ni jambo gumu sana kuendesha mazungumzo na watekaji nyara. Kawaida yanafanyika kupitia wapatanishi. Lakini Wakorea waliuvunja mwiko huo usiandikwa. Walizungumza na Wataliban ana kwa ana na hivyo kuwatambua kama kundi halali lenye mamlaka fulani nchini Afghanistan. Vilevile wamewapa ushindo fulani Wataliban ambao magaidi hao wanaweza kuutumia kuongeza wao kuungwa mkono, yaani makubaliano kuhusu jeshi la Korea Kusini kuondoka Afghanistan. Licha ya kwamba, kuondoa jeshi hilo ni jambo lililoamuliwa awali, bado Wataliban watatumia makubaliano haya kwa maslahi yao. Hivyo, serikali ya Korea Kusini iliiathiri serikali ya Hamid Karzai, na vilevile imeathiri msimamo wa serikali ya Ujerumani katika juhudi zake za kumwokoa habusu wa Kijerumani aliye bado mikononi wa watekaji nyara.”

Na kwa suala la pili linalozingatiwa na wahariri wa magazeti tunaelekea humu nchini Ujerumani ambapo kumezuka mjadala juu ya mpango wa waziri wa ndani Wolfgang Schäuble wa kupeleleza kwenye kompyuta za watumuhiwa wa mambo ya kigaidi. Chama cha Social Democrats kinapinga hatua hii na kusema kwamba utaratibu huu utaathiri uhuru wa wananchi. Mhariri wa “Mitteldeutsche Zeitung” lakini ana maoni mengine. Huu hapa uchambuzi wake:

“Wataalamu hawana uhakika utaratibu gani utawezekana kiteknolojia. Kwa upande wa kisiasa suali la msingi ni: Kwa kiasi gani serikali inapaswa kupunguza uhuru wa raia ili kuhakikisha usalama wa wote? Mahakama kuu ya katibu pia inashughulikia suala hilo, lakini inaonekena kama polisi itapewa ruhusa kuzipeleleza kompyuta. Tena ni lazima njia hii itumike, kwani magaida wanatumia teknolojia ya kompyuta katika mawasiliano yao. Kwa hivyo, hakuna tofauti kati ya kupeleleza mawasiliano ya simu na yale ya kompyuta.”