1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi wa chama cha AfD waleta mshangao

Sylvia Mwehozi
24 Septemba 2017

Vyama vya siasa vya hapa Ujerumani vimeshitushwa na matokeo ya uchaguzi wa Jumapili ambayo yamekuwa mazuri kwa chama cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD), baada ya kushinda asilimia 13.2 ya kura.

https://p.dw.com/p/2kd0x
Bundestagswahl | Elefantenrunde Gruppenbild
Picha: picture alliance/dpa/G. Breloer

AfD ilianzishwa mwaka 2013 kikiwa ni mkosoaji mkubwa wa Umoja wa Ulaya, lakini kimegeuza mwelekeo wake katika kuupinga Uislamu na uhamiaji katikati mwa ukosoaji mkubwa wa kitaifa kwa Kansela Angela Merkel, hasa kwa uamuzi wake wa kuwaruhusu mamia kwa maelfu ya wahamiaji kuingia Ujerumani baina ya mwaka 2015 na 2016.

Kwa asilimia 13.2 ya kura ilizopata chama hicho, AfD kinakuwa chama cha tatu kwa ukubwa bungeni na kukipatia nguvu zaidi ya vyama vingine maarufu - FDP kinachotetea biashara, die Grüne kinachotetea mazingira na kile cha mrengo wa kushoto, Die Linke.

Hofu ya kuongezeka kwa Waislamu

Matokeo ya awali yaliyokusanywa na taasisi ya utafiti ya Infratest dimap siku ya Jumapili yanaonesha kwamba asilimia 46 ya wapiga kura wa Ujerumani "wana hofu na kuongezeka kwa ushawishi wa Uislamu" hapa nchini.

Deutschland Bundestagswahl | Elefantenrunde
Viongozi wa vyama wakifanya majadiliano baada ya matokeo ya awaliPicha: picture-alliance/dpa/G. Breloer

Martin Schulz ambaye chama chake cha Social Democrats (SPD) kimeendelea kukubali kushindwa na muungano wa vyama ndugu vya kihafidhina, CDU/CSU vya Kansela Angela Merkel, na kuibuka kwa mbali katika nafasi ya pili, kimeyaelezea matokeo hayo kuwa "hasa ni ya huzuni."

Hii ni hatua ya kujitathmini," alisema Schulz akiongeza kwamba "ni wazi uamuzi wa kuwakaribisha wageni umeigawa nchi yetu. Hatua ya kuwaonea huruma binadamu inakuwa ni kitisho kwa wengine. Tumeshindwa kuwashawishi watu kwamba Ujerumani iko imara zaidi kutomuacha mtu nyuma."

Merkel bado anasimamia sera yake

Hata hivyo, Kansela Merkel anasema anataka "kurejesha imani ya wapiga kura kwa kusikiliza wasiwasi wao na hofu na kufanya siasa nzuri".  Kansela huyo amesema anao uhakika serikali itapatikana kabla ya Krismasi.

Akizungumzia matokeo ya uchaguzi huo, mgombea wa chama cha AfD, Alexander Gauland, mwenye miaka 76 alisema "tumefanikisha, tutaibadili nchi. Suala la kwamba sisi ni chama cha tatu chenye nguvu kunamaanisha kwamba serikali hii ni lazima ijiweke vyema. Tutawakimbiza.Tutamkimbiza Merkel au yeyote yule na tutachukua nchi yetu na taifa letu tena."

AfD kumshitaki Merkel bungeni

AfD Alice Weidel
Alice Weidel mgombea wa juu wa chama cha AfDPicha: Reuters/A.Schmidt

Alice Weidel, ambaye ni mgombea mwenza wa Gauland, alisema chama chake kitajaribu kuunda kamati ya bunge itakayofanya uchunguzi dhidi ya uvunjaji sheria uliofanywa na Merkel kuhusiana na mgogoro wa wakimbizi.

Weidel, ambaye aliteuliwa kulainisha msimamo na taswira ya AfD, alisema Merkel ni lazima afikishwe katika vyombo vya sheria kwa maamuzi yake ya kupindisha taratibu na kwa kusema kwamba maombi ya waomba hifadhi ni lazima yafanyike katika nchi ya kwanza wanakofikia katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Merkel, hata hivyo, amesema hatokwepa uchunguzi wa aina yoyote dhidi yake.

Miaka minne iliyopita, chama hicho kilishindwa kupata asilimia 5 kuingia katika bunge la shirikisho. Matokeo yaliyotolewa yanamaanisha kwamba chama hicho kitachukua viti vingi bungeni hadi kufikia 90 katika bunge lenye wabunge 630.

SPD imesema haitoungana tena na CDU na kumaanisha kwamba kitakuwa chama kikuu cha upinzani na AfD kitakuwa chama cha pili cha upinzani katika bunge.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef