1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi wa Erdogan bahati mbaya kwa Uturuki

13 Juni 2011

Chama cha Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kimeshinda kwa wingi mkubwa, uchaguzi wa bunge uliofanyika hiyo jana.

https://p.dw.com/p/RTHQ
epa02777144 Turkish Prime Minister Recep Tayyip Erdogan (L) and his wife Emine greet their supporters of Turkey's ruling Justice and Development Party (AKP) at the party headquarters in Ankara, Turkey, 12 June 2011. Turkey's ruling Justice and Development Party (AKP) was showing a strong early lead against the main opposition party in parliamentary elections on 12 June, local media reported. The conservative, mildly Islamist AKP was leading with about 55 per cent of votes, with fewer than 40 per cent of ballots counted, private broadcaster CNN Turk reported. The AKP had been widely expected to win a third term in office, but pre-election polls had predicted it would receive fewer than 50 per cent of votes, and possibly less than its 47 per cent share in the 2007 election. EPA/TOLGA BOZOGLU +++(c) dpa - Bildfunk+++
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan(kushoto) na mkewe EminePicha: picture-alliance/dpa

Lakini chama hicho, hakijafanikiwa kupata wingi wa theluthi mbili kama kilivyoazimia, ili kuweza kufanya mageuzi ya katiba bila ya kutegemea chama kingine. Kwa hivyo sasa, haitokuwa rahisi hivyo kusonga mbele na mpango huo. Mfumo wa kidemokrasia wa vyama mbali mbali hiyo jana katika uchaguzi wa bunge umeonyesha waziwazi kuwa chama cha Haki na Maendeleo AKP cha Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan kimeshinda kwa takriban asilimia 50 ya kura zilizopigwa. Vile vile asilimia 84 ya wapiga kura waliojitokeza kuchagua bunge jipya, imethibitisha ushindi halali wa kidemokrasia kwa chama cha AKP. Kwa mara ya tatu, chama hicho kimefululiza kuongeza kiwango cha ushindi wake. Katika mwaka 2002 kilipata asilimia 34 ya kura zilizopigwa; miaka minne baadae asilimia 46.5 na safari hii, kimejisombea takriban asilimia 50.

Chama kikuu cha upinzani, Jamhuri ya Umma, kimeshika nafasi ya pili baada ya kujinyakulia kiasi ya asilimia 25 ya kura, kikifuatwa na Nationalist Action Party, chenye siasa kali za mrengo wa kulia, kilichopata asilimia 13 ya kura. Chama cha Amani na Demokrasia BDP, kinachotetea maslahi ya Wakurdi nchini Uturuki kimefanikiwa kupata viti 35 bungeni. Miongoni mwa washindi wao ni wakosoaji kadhaa wa Erdogan, wasio wa Kurdi na wangali kizuizini wakingojea kesi zao. Watu hao wamezuiliwa kwa madai kuwa waliunga mkono njama ya mapunduzi.

Mambo gani yaliyompatia Erdogan ushindi huu wa tatu katika kipindi cha miaka tisa? Uchumi wa Uturuki unaendelea kukua tangu miaka kadhaa. Kasi ya mageuzi yaliyoazimia kufuata maadili na kanuni za Umoja wa Ulaya imepungua baada ya nchi hiyo mwanachama wa NATO kuvunjika moyo kuhusu uwezekano wa kuwa mwanachama katika umoja huo. Maendeleo kama kuimarishwa uhuru wa watu binafsi na taasisi katika kila tabaka, yamesukumwa nyuma.

Ushindi mkubwa wa Erdogan ni bahati mbaya kwa Uturuki. Miaka hii iliyopita, amezidi kukataa ushauri na wala haoni haya kuwatangaza wapinzani wake kama maadui wa taifa. Kwa bahati nzuri chama chake cha AKP hakijafanikiwa kupata viti 330 bungeni, kwa hivyo hakitoweza kubadili katiba bila ya kuafikiana na upinzani. Kwa hivyo, hivi sasa Erdogan, hatoweza kufanya mageuzi ya kutaka kuifanya Uturuki jamhuri yenye rais alie na madaraka zaidi.

Licha ya ushindi mkubwa, Uturuki itakabiliana na wakati mgumu. Chama cha AKP kitazidi kuwashinikiza wapinzani wake. Uhuru wa vyombo vya habari utaendelea kubanwa na dini itapewa kipaumbele, kinyume na katiba inayotenganisha dini na siasa. Kwa hivyo, Uturuki yenyewe, itaupa Umoja wa Ulaya sababu ya kukataliwa uanachama.

Mwandishi: Güngör,Baha/ZPR

Mhariri: Miraji, Othman