1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushirika kumng'owa Netanyahu Israel

11 Desemba 2014

Waziri wa zamani wa sheria wa Israel Tzipi Livni na kiongozi wa upinzani wa kundi la sera za mrengo wa kati kushoto kuungana katika uchaguzi ujao ili kumn'gowa madarakani Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

https://p.dw.com/p/1E2Y7
Waziri wa zamani wa sheria wa Israel Tzipi Livni akiwa na kiongozi wa chama cha Labour Isaac Herzog.
Waziri wa zamani wa sheria wa Israel Tzipi Livni akiwa na kiongozi wa chama cha Labour Isaac Herzog.Picha: picture-alliance/dpa/Jim Hollander

Kufuatia miezi kadhaa ya malumbano ya ndani kuhusu jinsi ya kushughulikia mazungumzo ya amani yaliokwama na Wapalestina yaliodhaminiwa na Marekani,Netanyahu wiki iliopita alimtimuwa Livni kutoka baraza lake la mawaziri na hiyo kuvunja serikali tawala ya mseto ya kihafidhina inayopendelea kuitishwa kwa uchaguzi wa mapema.

Livni aliuambia mkutano wa waandishi wa habari Jumatano (10.12.2014) ambao umehudhuriwa pia na Isaac Herzog wa chama cha Labour kwamba yuko hapo kuunda kikosi mchanganyiko ambacho kitabadili serikali katika taifa la Israel.

Uchunguzi wa maoni ulitabiri kwamba chama cha mrengo wa kulia cha Netanyahu cha Likud kitashinda uchaguzi huo uliopangwa kufanyika hapo tarehe 17 mwezi wa Machi kwa kujipatia kama viti 22 kati ya viti 120 vya bunge. Vikiwania uchaguzi huo kwa tiketi tafauti chama cha Labour na kile cha Livni cha mrengo wa kati cha Hatnuah vimeonekana viko nyuma ya Likud.

Kushinda kwa tiketi ya pamoja

Lakini uchunguzi wa maoni uliofanywa Disemba nne na gazeti la Globes na ule wa Disemba saba uliofanywa na kituo cha televisheni cha bunge umegunduwa kwamba vyama hivyo vikigombea kwa pamoja vitakipita chama cha Likud kwa viti 23 hadi 24.

Waziri wa zamani wa sheria wa Israel Tzipi Livni.
Waziri wa zamani wa sheria wa Israel Tzipi Livni.Picha: Gali Tibboni/AFP/Getty Images

Herzog amewaambia waandishi wa habari iwapo watafanikiwa kuunda serikali atatumika kama waziri mkuu katika nusu ya kipindi cha kwanza na watabadilishana wadhifa huo na Livni katika kipinchi cha pili.

Ameahidi kubadilisha hali ya kutengwa kimataifa kwa Israel kutokana na kukwama kwa mazungumzo na Wapalestina na sera za utaifa na kuleta usalama badala ya hofu na mazungumzo badala ya chuki.

Muungano wawekewa mashaka

Baadhi ya wachambuzi wana wasi wasi iwapo muungano utaweza kufanya kazi.Livni ambaye asili yake alikuwa mwanachama wa Likud amebadilisha vyama mara tatu tokea mwaka 2005 na kushindwa mara tatu kuupata wadhifa wa uwaziri mkuu.

Hayo yanajiri wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akitazamiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Rome hapo Jumapili kwa mazungumzo juu ya masuala mbali mbali ya mzozo wa Mashariki ya Kati ambayo hivi sasa mapendekezo yake yamesambazwa Umoja wa Mataifa hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki hapo jana amekanusha kwamba ziara hiyo ina uhusiano wowote ule na uchaguzi unaokuja wa Israel.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.Picha: Reuters

Psaki amekaririwa akisema mjini Washington "Hatwendi Israel.Ni dhahir kwamba juhudi za diplomasia na utekekelezaji wa sera za kigeni ni mambo yanayohitajika kufanyika hata katika miezi kabla ya uchaguzi."

Kwa upande mwengine Wapalestina wameilaumu Israel kwa kifo cha waziri asiyekuwa na wizara maalum Ziad Abu Ain aliyefarika hapo jana kwa kile walichoeleza kutokana na kuvuta hewa ya gesi ya kutowa machozi na kipigo wakati wa purukushani na wanajeshi wa Israel kaskazini mwa Ramallah.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mharir: Mohammed Abdul-Rahman