1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushirika mpya kati ya Afrika na Ulaya

3 Aprili 2014

Viongozi wa Afrika na Umoja wa Ulaya wamekuwa na mazungumzo juu ya matumizi ya nguvu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo wanajeshi wa kulinda amani wameshindwa kukomesha mzozo kati ya Wakristo na Waislamu.

https://p.dw.com/p/1BbJV
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika Brussels. (02.04.2014)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika Brussels. (02.04.2014)Picha: Reuters

Viongozi wa Afrika na Umoja wa Ulaya jana wamekuwa na mazungumzo kuhusiana na matumizi ya nguvu yenye kutowa taswira ya kutisha Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo wanajeshi wa kulinda amani wameshindwa kukomesha mzozo wa umwagaji damu kati ya Wakristo na Waislamu.

Ufaransa na Ujerumani zimetangaza ushirika mpya kwa Afrika katika mkutano huo uliohudhuriwa na takriban viongozi 80 wa mabara hayo mawili, shirika ambao unakusudia kuendeleza amani na maendeleo halikadhalika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema kwamba wanataka kutumia urafiki wao ndani ya bara la Afrika lenyewe na ameongeza kusema kwamba ni kutokana na Ujerumani kwamba Umoja wa Ulaya hatimae umeweza kutangaza kuzinduliwa kwa utumaji wa wanajeshi 800 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema Ujerumani na Ufaransa zinatakuwa kuwa ingini katika suala la maendeleo halikadhalika usalama. Merkel amesema wanawekeza Afrika ili Afrika likiwa bara linalojiamini liweze kuyapatia ufumbuzi wenyewe matatizo yake.

Ikicheleweshwa kutokana na kushindwa kupata wanajeshi wa kutosha na ndege kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya,kuzinduliwa kwa operesheni hiyo ya Umoja wa Ulaya kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kumetangazwa katika mkesha wa mkutano huo wa Kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika unaomalizika leo hii.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika Brussels. (02.04.2014)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika Brussels. (02.04.2014)Picha: Reuters

Ujerumani imekubali kutowa ndege za uchukuzi, wakati Georgia,Uhispania,Estonia,Finland ,Italia , Latvia,Poland na Ureno zimekubali kutowa wanajeshi na Uingereza,Luxembourg na Sweden zitatowa msaada wa vifaa na usafirishaji.

Afrika ya Kati yajadiliwa

Hali ya machafuko Jamhuri ya Afrika ya Kati imezidi kuwa mbaya ambapo viongozi wa nchi wanachama 54 wa Umoja wa Afrika na 28 wa Umoja wa Ulaya imebidi wakutane na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kujadili mzozo wa nchi hiyo.

Ban ameonya kwamba hali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati inaweza kugeuka na kuwa mauaji ya halaiki kufuatia repoti za Umoja wa Mataifa za kukatwa kichwa kwa mtoto,ulaji wa nyama ya binaadamu na kuenea kwa mauaji holela yanayofanywa na umma wa watu.

Ban anataka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liidhinishe wanajeshi wa kulinda amani 12,000 kuchukuwa nafasi ya wanajeshi 8,000 wa Afrika na Ufaransa walioko nchini humo hivi sasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika Brussels. (02.04.2014)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika Brussels. (02.04.2014)Picha: Reuters

Wakati wajumbe wakianza kujadili suala la uhamiaji biashara na usalama na matatizo mengine yalioko barani humo viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesisitiza kwamba wanataka kuwepo kwa ushirika utakaozingatia usawa baina ya pande hizo.

Tafauti na mikutano mengine ya kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika suala la msaada wa maendeleo halikudhibiti mkutano huo badala yake viongozi hao wametaka kuboresha uhusiano wa kibiashara na kutambuwa uwezo wa ukuaji ulioko barani Afrika.

Biashara baina ya mabara hayo mawili imeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni. Hapo mwaka 2012 Umoja wa Ulaya uliagizia bidhaa za Afrika zenye thamani ya euro bilioni 187 wakati Afrika ilinunuwa bidhaa zenye thamani ya euro 152 kutoka mataifa ya Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Yusuf Saumu