1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushirikiano Mpya wahitajiwa kutimiza Malengo ya Milenia

P.Martin6 Julai 2007

Ushirikiano mpya unahitajiwa kati ya mataifa tajiri na masikini,ili kuweza kutimiza malengo ya Umoja wa Mataifa kupunguza umasikini,ifikapo mwaka 2015.Hayo ni kwa mujibu wa afisa mmojawapo aliesaidia kupanga Malengo ya Maendeleo ya Milenia.

https://p.dw.com/p/CHBX

Jan Vandemoortele,ambae hivi sasa anaongoza Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa nchini Pakistan, hujieleza kama ni mkunga mmojawapo wa malengo manane yaliyokubaliwa na viongozi wa kimataifa kwenye mkutano wa kilele hapo mwaka 2000.

Kuambatana na Malengo ya Maendeleo ya Millenia au MDG,mataifa yaliyotia saini yanawajibika kupunguza kwa theluthi mbili kiwango cha vifo vya watoto.Wakati huo huo idadi ya wanawake wanaofariki katika uzazi,ipunguzwe kwa asilimia 75.

Viongozi hao wa kimataifa vile vile waliahidi kuwa mfumo wa biashara ya kimataifa,utabadilishwa ili usaidie kupunguza umasikini.

Lakini Vandermoortele anasema,baadhi ya madola makuu hayapo tayari kuachana na fikra za zamani,ili kuweza kutimiza malengo yaliyowekwa katika kipindi kilichokubaliwa yaani ifikapo mwaka 2015.Akieleza zaidi amesema,nchi za magharibi hazipo tayari kubadili msimamo wao kuwa kwanza nchi zinazoendelea zifungue masoko yake kwa bidhaa za viwandani kutoka Magharibi,na baadae ndio nchi za Magharibi zitafungua masoko yake kwa mazao ya kilimo kutoka nchi zinazoendelea.

Ukweli huo anasema,ulidhihirika kwenye mkutano wa Doha kuhusu biashara duniani.Wakati wa majadiliano hayo,Umoja wa Ulaya na Marekani zilishikilia kwamba nchi nyingi zinazoendelea zipunguze kwa kiwango kikubwa ushuru unaotozwa kwa bidhaa zinazoingizwa,licha ya kuwa ushuru huo huchangia sehemu muhimu ya pato la nchi zinazoendelea.Vile vile ushuru wa aina hiyo huweza kuvisaidia viwanda chipukizi,kushindana na bidhaa za kigeni.

Kwa maoni ya afisa huyo wa Umoja wa Mataifa,uhusiano wa sasa kati ya nchi tajiri na masikini si imara,kwa sababu msingi ni kwamba upande mmoja una pesa na wa pili hupokea pesa hizo.Uhusiano huo wapaswa kufanyiwa mabadiliko, ili pande hizo mbili ziweze kubadilishana fikra na mawazo,badala ya kubadilishana pesa.

Wakati huo huo Vandemoortele amesema,sababu mojawapo kuu ya kutofanikiwa miradi yenye azma ya kupunguza umasikini ni kwamba,miradi hiyo haiwanufaishi vya kutosha watu walio masikini sana.Badala yake wenye hali bora ndio wamenufaika kuliko waliokuwa na shida zaidi.