1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushirikiano uimarishwe Ulaya

Prema Martin/afpe 26 Januari 2012

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika hotuba yake ya ufunguzi katika kongamano la kiuchumi duniani mjini Davos, alisisitiza kuwa Ulaya itaendelea kuongoza kiuchumi duniani, ikiwa tu itaimarisha ushirikiano wake.

https://p.dw.com/p/13q7G
German Chancellor Angela Merkel, delivers the opening address at the World Economic Forum in Davos, Switzerland, Wednesday, Jan. 25, 2012. The overarching theme of the Meeting, which will take place from Jan. 25 to 29, is "The Great Transformation: Shaping New Models". (Foto:Michel Euler/AP/dapd).
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, asisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano UlayaPicha: AP

Merkel amewaonya viongozi na wataalamu wa uchumi katika kongamano hilo kuwa ushirikiano huo usipopatikana, basi mkutano wa Davos katika mji huo wa mapumziko milimani Uswisi, utabakia kama likizo nzuri tu. Kwa kweli ujumbe wa Merkel katika hotuba yake ya hapo jana, haukutofautiana na msimamo wake wa kawaida, lakini umesaidia kuchochea hisia miongoni mwa viongozi wa Ulaya juu ya umuhimu wa kuchukuliwa hatua yo yote, ili kusaidia kuiokoa sarafu ya euro. Merkel ameahidi kuchukua hatua zinazohitajiwa kuinusuru euro lakini amesema, kunahitajiwa ushirikiano mkubwa zaidi barani Ulaya, utakaosaidia kupata nafasi mpya za ajira na kuimarisha ukuaji wa kiuchumi. Akaongezea:

"Kile ambacho hatutaki ni kujikuta katika hali ya kuahidi kitu ambacho hatimae hatuwezi kukitekeleza. Kwani Ujerumani ikiahidi kitu kwa niaba ya nchi zote na ikishindwa kukitekeleza kwa sababu ya vishindo katika masoko, hapo Ulaya itajikuta katika hali ambayo si salama."

Ujerumani imeshika usukani, kuongoza mpango wa kuinusuru euro, kwani barani Ulaya inaongoza kiuchumi. Na Ulaya ndio mada kuu katika kongamano la Davos, kwani wengi wana hofu kuwa uchumi wa kimataifa utadorora upya, ikiwa mzozo wa euro hautopatiwa ufumbuzi haraka.Tangu miezi kadhaa Ujerumani inazitaka nchi zenye madeni makubwa kupunguza matumizi ya serikali. Bila shaka, hiyo itawaathiri raia, lakini hilo ndio sharti la kupewa msaada wa fedha, utakaopunguza mzigo wa madeni. Hata hivyo, kuna wengi wanaoamini kuwa hiyo haitosaidia, ikiwa hatua za kubana matumizi zitaathiri ukuaji wa kiuchumi na hivyo nchi hizo kushindwa kuyalipa madeni yaliyobaki.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wataalamu wa uchumi katika kongamano la Davos, wanahisi kuwa mfumo wa kibepari wa nchi za magharibi uliotumika kwa miongo kadhaa, sasa unahitaji kufanyiwa mageuzi. Mzozo wa kiuchumi unaoendelea tangu mwaka 2008 na kuathiri uchumi barani Ulaya, unawashinikiza wanasiasa kuzingatia mfumo mpya, huku ikidhihirika kuwa nchi za Asia na Amerika ya Kusini zinainukia kiuchumi. Viongozi 40 kutoka nchi mbali mbali na wataalamu wa uchumi 2,500 wanahudhuria mkutano huo wa Davos utakaomalizika jumapili ijayo.