1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji mapigano Aleppo warefushwa kwa masaa 72

7 Mei 2016

Usitishaji wa mapigano wa muda katika eneo la mapigano nchini Syria katika mji wa Aleppo umerefushwa kwa masaa mengine 72 kuanzia leo Jumamosi(07.05.2016),wakati mapigano yakiendelea upande wa kusini.

https://p.dw.com/p/1IjTP
Syrien Zerstörung in Aleppo
Magofu ya mji wa AleppoPicha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Urefushaji wa kusitisha mapigano kwa ajili ya Aleppo unakuja wakati shutuma za kimataifa zinaongezeka kuhusiana na mashambulizi mabaya ya anga yaliyosababisha umwagikaji wa damu katika kambi kwa ajili ya watu waliokimbia makaazi yao kaskazini mwa Syria, ambayo serikali na mshirika wake Urusi wamekana kuhusika nayo.

Syrien Aleppo Panzer
Wapiganaji wanaoipinga serikali nje ya mji wa AleppoPicha: picture alliance/abaca/B. el Halebi

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema usitishaji huo tete wa mapigano umerefushwa "ili kuzuwia hali kuwa mbaya zaidi" dakika chache kabla ya usitishaji wa awali wa saa 48 kwa ajili ya mji huo kumalizika.

"Hali ya utulivu katika jimbo la Latakia na mji wa Aleppo umerefushwa kutoka usiku wa manane Mei 7 kwa masaa 72," wizara ya ulinzi imesema katika taarifa.

Marekani yathibitisha

Marekani -- ambayo imekuwa ikifanyakazi pamoja na Urusi kuweka mbinyo kwa serikali kuzuwia ghasia na kufufua makubaliano ya kihistoria ya nchi nzima ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Februari --- pia ilithibitisha kurefushwa huko.

Syrien Krieg Kämpfe in Aleppo
Watu wakipita katika vifusi vya majengo yaliyoshambuliwa mjini AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

"Wakati tunakaribisha urefushaji huu , lengo letu ni kupata kufikia mahali ambako hatutakuwa tunahesabu masaa na kwamba kusitishwa kwa uhasama kunaheshimiwa nchi nzima Syria," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani John Kirby.

Jumuiya ya kimataifa ina matumaini kwamba kupungua kwa mapigano kunaweza kuimarisha mazungumzo yanayolegalega ya amani kumaliza miaka mitano ya vita ambavyo vimeuwa zaidi ya watu 72,000 na wengine milioni kadhaa kukimbia makaazi yao.

Utulivu umerejea katika mitaa ya Aleppo baada ya kusitisha mapigano kuanza usiku wa manane siku ya Alhamis, na kuwapa wakaazi unafuu kidogo kutoka wiki mbili za mapigano ambayo yamesababisha kiasi ya raia zaidi ya 280 kuuwawa.

Syrien Zerstörung bei Aleppo
Majengo yaliyoharibiwa mjini AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

Mapigano ya hapa na pale

Lakini kusini mwa mji huo, mapigano ya hapa na pale baina ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa Jihadi pamoja na washirika wao yamewauwa zaidi ya watu 70 kutoka kila upande, shirika linaloangalia haki za binadamu nchini humo limesema jana Ijumaa,(06.05.2016).

Al-Nusra na washirika wao wapiganaji wa itikadi kali ya Kiislamu walikamata kijiji cha Khan Tuman na vijiji vinavyozunguka eneo hilo chini ya masaa 24, kwa mujibu wa shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza, baada ya majeshi yanayoiunga mkono serikali kuwafurusha kutoka eneo hilo mwezi Desemba.

Syrien Aleppo Bürgerkrieg Zerstörung
Mji wa Aleppo baada ya mashambulizi ya angaPicha: picture-alliance/dpa/Z. Al Shimale

Wanawake na watoto wanaripotiwa kuwa miongoni mwa wale waliouwawa katika mashambulizi ya Alhamis katika kambi karibu na mpaka na Uturuki, ambapo pia watu 50 wamejeruhiwa.

Mamun al-Kahatib , mkurugenzi wa shirika la habari linalounga mkono waasi mjini Aleppo, ameshutumu kile alichosema kuwa ni "ndege za utawala" kwa kushambulia kambi hiyo katika kijiji cha Al-Kammouna siku ya Alhamis -- shutuma ambazo serikali mjini Damascus inakana.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Sudi Mnette