1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji mapigano ungalipo - Moallem

Mohammed Khelef
26 Septemba 2016

Licha ya kuyashambulia vikali maeneo yanayoshikiliwa na waasi katika mji wa kaskazini wa Aleppo, serikali ya Syria inasema bado makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na Urusi yangalipo.

https://p.dw.com/p/2QbRl
Syrien Außenminster Walid al-Muallim
Picha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Mayadeen chenye makao yake jijini New York, Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid Moallem, amesema hivi leo (Septemba 26) kwamba makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Urusi na Marekani, na kuonekana kuvunjika wiki nzima sasa, bado yapo hai na serikali yake inayaheshimu. 

Kauli hiyo ya Moallem inakuja licha ya taarifa za mashambulizi makali ya wiki nzima ya ndege za serikali kwenye maeneo yanayoshikiliwa na waasi mjini Aleppo, ambapo hadi sasa watu 240 wameshauawa.

Wafanyakazi wa huduma za uokozi waliripoti mashambulizi mapya asubuhi ya leo, wakiyaelezea kuwa ni mabaya na makubwa zaidi kuwahi kufanyika kwenye eneo hilo tangu vita kuanza miaka mitano iliyopita.

Iran yapinga usitishaji mapigano na 'magaidi'

Kwa upande mwengine, Iran, ambayo ni mshirika wa utawala wa Assad kwenye vita hivi, imesema hakuna sababu ya kuendelea na makubaliano ya kusitisha mapigano, madhali tu wale iliowaita "magaidi" wanaendelea kuyadhibiti maeneo muhimu.

Syrien Aleppo Trümmer nach einem Luftangriff
Mtu akitembea kwenye kifusi cha jengo lililoangushwa kwa mashambulizi ya anga ya jeshi la Syria katika kitongoji kinachodhibitiwa na waasi mjini Aleppo siku ya tarehe 25 Septemba 2016.Picha: Reuters/A.Ismail

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Bahram Ghasemi, amesema mataifa yenye nguvu na jirani mwa Syria yanajaribu kupitisha muda ili makundi hayo yazidi kujiimatisha na kuwapa nafasi ya kuja juu upya. 

Spika wa Bunge la Syria, Bi Hadiya Khalaf Abbas, ambaye yuko ziarani nchini Iran, amerejelea msimamo wa serikali ya nchi yake kukataa kupangiwa nini cha kufanya na mataifa ya kigeni.

"Sisi ni nchi yenye mamlaka yake na ina rais wake ambaye amechaguliwa na watu wa Syria na kuthibitishwa na kuridhiwa na na taifa la Syria kwa kuwa anapambana, na anawapenda watu wake. Miaka sita ya mapambano haya inathibitisha hilo." Alisema Spika Hadiya jijini Tehran.

Hayo yakiendelea, hali kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inazidi kupamba moto.

Kikao cha dharura kilichoitishwa jana kujadili mashambulizi dhidi ya mji wa Aleppo kilikuwa cha kutupiana maneno na kushutumiana kati ya Urusi na Marekani na washirika wake kwenye Baraza hilo.

Ambapo Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo, Samantha Power, alisema "Inachofanya Urusi nchini Syria ni ushenzi na kufadhili ugaidi na sio kupambana nao," wenzake wa Ufaransa na Uingereza wamesema kinachoendelea sasa Aleppo ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Saumu Yussuf