1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji wa mapigano kati ya Israel na Hamas waanza chini ya kiwingu cha mashaka.

Mohamed Dahman19 Juni 2008

Israel na Hamas zimesitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza lakini matarajio ya amani yako chini ya mashaka juu ya muda gani usitishaji huo wa mapigano chini ya usuluhishi wa Misri utaweza kudumu.

https://p.dw.com/p/EMs0
Kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza Mahmoud Zahar kushoto akitangaza mjini Gaza kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas.Picha: AP

Muda mfupi tu baada ya suluhu hiyo kuanza kufanya kazi baada ya alfajiri leo hii shambulio la kombora la Israel limemuuwa mpiganaji mmoja wa Kipalestina na kumjeruhi mwengine karibu na uzio wa mpakani na Israel katikati ya eneo la Ukanda wa Gaza.

Usitishaji huo wa mapigano umeanza kufanya kazi saa 12 asubuhi kufuatia siku nyengine ya mashambuliano ya mpakani. Madarzeni ya makombora ya Kipalestina na mabomu yanayovurumishwa kwa mizinga yalipiga kusini mwa Israel lakini bila ya kusababisha uharibifu mkubwa na mashambulizi ya anga ya Israel yamejeruhi wapiganaji wa Kipalestina huko Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ameliambia gazeti la Australia la Sydney Morning Herald kwamba makubaliano hayo ya amani ni fursa ya mwisho kwa wanamgambo hao wa Kipalestina kuepusha kujiingiza tena kijeshi kwa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Olmert amesema mkakati wa Hama kwanza hautaki kutambuwa haki ya kuwepo kwa taifa la Israel na kwamba itikadi kali na misimamo mikali ya kidini ni adui wa amani.

Katika hotuba hapo jana Olmert alitahadharisha kwamba makubaliano hayo na Hamas kundi ambalo liliteka eneo la Gaza kutoka kwa vikosi vya kundi la Fatah la Rais Mahmoud Abbas anayeungwa mkono na mataifa ya magharibi mwaka mmoja uliopita ni lege lege na yanaweza yasidumu kwa muda mrefu.

Mark Negev msemaji wa serikali ya Israel amesema Israel imeamuwa kukubali mapendekezo ya Misri na ni matumaini yao ya dhati kabisa kwamba kuanzia leo raia wao walioko kusini mwa nchi hawatokuwa tena wahanga wa mashambulizi hayo yanayoendelea ya maroketi na makombora kutoka kwa magaidi walioko Ukanda wa Gaza na kwamba watakuwa na kipindi kipya cha amani na utulivu.

Kwa Hamas kusitisha uhasama na Israel kunatazamia kuwapa afueni fulani kutokana na vikwazo vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kunaweza kukawasaidia kupata uhalali kutoka kwa mataifa ya magharibi na upatanishi na Abbas ambaye yuko mbioni kutafuta amani na Olmert katika mazungumzo yanayodhaminiwa na Marekani.

Kitengo cha wapiganaji cha Hamas kimesema katika taarifa iliochapishwa muda mfupi baada tu ya kuanza kutekelezwa kwa usitishaji wa mapigano kwamba iko tayari kabisa kufanya shambulio la kijeshi ambalo litautingisha uzayuni iwapo hawatozingatia vipengele vyote vya usitishaji huo wa mapigano.

Suluhu hiyo inakuja wakati Waziri Mkuu wa Israel Olmert pia akishughulikia suala la kubadilishana wafungwa na wapiganaji wa kundi la Hezbollah wa Lebanon na mazungumzo yasio ya moja kwa moja na Syria halikadhalika wazo la kuwa na amani na Lebanon.