1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utamaduni: Muziki wa Kandongo kamu nchini Uganda

18 Juni 2012

Unapozungumzia historia ya muziki nchini Uganda bila kuitaja Kadongo kamu, basi historia hiyo haijakamilika.

https://p.dw.com/p/15FmE
Sonnenaufgang über dem Morgennebel im Westen von Uganda.
Uganda - LandschaftPicha: picture alliance / Ton Koene

Huu ndiyo muziki wa kwanza kabisa nchini humo ambao, kwa maneno mengine, unaweza kusema ndiyo muziki wa asili wa nchi hiyo. Kadongo Kamu ni neno la kiganda linalomaanisha Gita moja. Ili kufahamu kwanini muziki huu ulipewa jina hili mtu laazima ajue muundo wa mtindo wenyewe wa muziki ambao unategemea zaidi gita moja la Besi. Ingawa siku hizi vifaa vingine hutumika katika kuucheza muziki wa kadongo kamu, lakini ladha ya kweli ya muziki huu inatokana na gita la besi kama mpangilio wa ala katika muziki, na huo ndiyo msingi wa jina la muziki wa kadongo kamu.

Mathias Walukagga ni mmoja wa wasanii maarufu wa muziki wa Kadongo kamu nchini Uganda, na ingawa anakiri kuwa yeye aliukuta muziki huu ukiitwa kadongo kamu, anakubali kuwa asili ya neno hili ni matumizi ya gita moja kwa wanzilishi wake.

Lakini kadiri siku zilivyokwenda, muziki huu ulianza kuboreshwa kwa kuongezewa vyombo vingine kama vile Jazz, tarumbeta, gita nyingine n.k. Lakini mwanzo ilikuwa gita moja na sisi tulivyokuja ingawa tuliongeza vyombo vingine, lakini jina lilibako vile vile, hatuna namna ya kuweza kulibadilisha.

Kiongozi wa chama cha National Front Marine Le Pen. Alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais, lakini ameshindwa ubunge.
Gita la besi ndiyo chombo kikuu katika muziki wa kadongo kamu.Picha: AP

Kwa nini gita la besi hupendelewa?
Ili kufahamu kwa ni gita la besi ndiyo chombo kinachopendelewa zaidi, ni laazima kwanza kufahamu utamaduni wa ngoma za kiganda ambako muziki huo ndiko ulikoanzia. Kuna aina ya ngoma na muziki ujulikanao kama Bakisimba katika muziki asili wa kiganda na hii ni moja ya ngoma maarufu zaidi katika muziki wa asili nchini Uganda.

Ngoma inayotumika katika muziki huu wa bakisimba ni kubwa na yenye besi inayotengeneza ala za muziki ambazo zinaweza kutengenezwa kwa urahisi zaidi kwa kutumia gita la besi. Wasanii wa kwanza kufanya muziki huu walihamasishwa na midundo ya ngoma hii ya bakisimba na hivyo wakaanza kutumia gita za besi kutengeneza ala hizo bila kuwa na ngoma. Hii iliwawezesha kusafiri kati ya miji na vijiji huku wakicheza muziki wao na kufikisha ujumbe wenye maana na wa kujirejea kwa hadhira mbalimbali, na huo ukawa ndiyo mwanzo wa safari ya muziki huu.

Ilikuwa mara nyingi mpiga gita ndiyo mwenye kuimba na hivyo unakuta waimbaji wa muziki wa kadongo kamu vilevile ni wapiga gita wazuri. Muundo wa nyimbo haujainishwa vizuri na wakati mwingine unaonekana kama utenzi mrefu wa aina fulani. Viitikio ni virefu na vyenye kutatanisha na hakuna kujirudia. Wakati mwingine sauti si tamu kama aina nyingine za muziki. Si muziki kwa ajili ya kucheza, bali ni muziki kwa ajili ya kusikiliza. Ndiyo maana waimbaji wanakuwa na akili sana na wanaweza kuimba mashairi yenye kuchekesha na yenye kuchokoza mawazo, vyote katika wimbo mmoja.

Alama ya muziki.
Alama ya muziki.Picha: Fotolia/Freesurf

Kama ilivyo kwa muziki wa asili ambako ndiko ulikotokea, muziki wa kadongo kamu unajikita zaidi katika kusimulia hadithi. Mada mara nyingi huwa ni juu ya umaskini, mateso, kifo na matatizo ya kila siku ya kimaisha. Ni kutona na sababu hizi, muziki huu ni maarufu sana miongoni mwa watu wenye umri mkubwa, wakulima na wenye vipato vya chini ambako viwango vya umaskini viko juu zaidi na kuna uwezo mkubwa wa kuvuta hisia kutokana na mada zinazoimbwa. Lakini zipo tofauti nyingi kati ya kadongo kamu na muziki mwingine.

Tofauti ya kadongo kamu na muziki mwingine
Tofauti ya kadongo kamu na muziki mwingine ni kwamba, nyimbo zake zinakuwa ndefu kuliko aina nyingine za muziki, na pili muziki huu unaelimisha zaidi na unakuta kwamba mashabiki wanaokuja katika show zetu ni watu wenye heshima zao, unaweza kumuona mtu kaja kwenye show amevalia suti na ameleta hata familia yake, anasema Walukagga.

Msanii huyo aliyejipachika jina la Ever Smart anasema katika muziki wa kadongo kamu hakuna kushindana na badala yake wasanii wanashirikiana na kila mmoja hupenda kuusikiliza muziki wa mwenzie. Anasema kila msanii anatunga kuhusiana na mada tofauti na wala siyo muziki wa kujibizana kama ilivyo kwa Hip Hop ambako msanii moja anatunga kibao na mwingine anatunga kujibu mapigo. Nilimuuliza Walukagga kama hawashindani kati yao, je wanashindana na muziki wa kizazi kipya?

Muziki wa kadongo kamu hujikita zaidi katika mambo yanayogusa jamii kwa ujumla.
Muziki wa kadongo kamu hujikita zaidi katika mambo yanayogusa jamii kwa ujumla.Picha: AP

"Hapana, sisi hatutaki mashindano na wala hatutaki muziki wao na wala hatuutamani kwa sababu wao wanaoshindana, akiimba wimbo unadumu kwa mwezi mmoja au mitatu na baadae atalaazimika kutunga mwingine. Lakini mimi kwa mfano nikiende kwenye show, mashabiki wanaanza kuulizia wimbo niliopiga miaka saba iliyopita. Lakini hawa kila baada ya miezi mitatu wanatoa nyimbo mpya na hii inamaanisha kwamba nyimbo zao hazina maana."

Wasanii wa kwanza wa kadongo kamu
Mtu wa kwanza mashuhuri katika muziki wa kadongo kamu alikuwa akiitwa Fred Masagazi katika miaka ya sitini. Masagazi anachukuliwa kuwa ndiye baba wa muziki wa kadongo kamu. Chapa yake ya muziki wenye kuelemisha ilimpatia mashabiki wengi na ni moja wa wasanii wachache sana walioshiriki harakati za Uhuru wa Uganda mwaka 1962.

Elly Wamala alikuwa mmoja wa wanzilishi pia wa muziki huu. Hawa walifuatiwa na wengine kadhaa ambao waliuendeleza muziki wa kadongo kamu. Herman Basudde alikuwa mwanamuziki maarafu sana wa kadongo kamu katika miaka ya 80 na 90. Dan Mugula ni moja wa wanzilishi wachache wa muziki huu walio hai. Fred Sebatta na marehemu Paul Kafeero walikuwa maarufu sana katika miaka ya 90.

Umaskini na hali ngumu ya maisha ni mada kuu katika muziki wa kadongo kamu.
Umaskini na hali ngumu ya maisha ni mada kuu katika muziki wa kadongo kamu.Picha: DW

Kafeero anasifiwa kuwa mtu aliyekuwa na uwezo zaidi katika historia ya muziki huu na kibao chake cha Walumbe Zaaya ndiyo moja ya nyimbo bora na maarufu zaidi nchini Uganda. Walukagga anakubali Kafeero alikuwa bora zaidi.

"Mtu wa kigezo katika safari yangu ya Muziki alikuwa ni Paul Kafeero na mwingine alikuwa anaitwa Mabirizi sikuwahi kumuona ila muziki wake naupenda sana n amara nyingi nausikiliza, ndiyo watu wawili hao," anasema Walukagga.

Jitihada za kutunza muziki huu
Ingawa wengi wa wanzilishi wa muziki hawako duniani tena, jitihada mbalimabli zinafaywa ili kuutunza. Moja ya mbinu zinatotumiwa kwa sasa ni wasanii kurudia nyimbo za wale waliyokwisha fariki ambazo wanazirekodi katika video lakini kwa kutumia sauti za wahusika. Pia katika mtandao wa Youtube sasa hivi nyimbo hizi zinapatikana kwa wingi kwa njia ya sauti na video.

Muziki huu bado unapendwa sana na watu watiifu kwa utamaduni katika eneo la Buganda, na hali hii inawahakikishia waimbaji wake kuwa kutakuwa na hadhira daima kwa muziki wa kadongo kamu, kama inavyoonekana sasa kwa wasanii kama vile Fred Sebaale, Mathias Walukagga ambao bado wanaendelea kushika nafasi za juu nchini humo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Othman Miraji