1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utambue muungano wa Amani

4 Machi 2013

Muungano wa Amani chini ya uongozi wake Naibu Waziri Mkuu, Musalia Mudavadi, unatoa ahadi za kuwapatanisha makabila yote nchini Kenya endapo utashinda kwenye zoezi la uchaguzi mkuu nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/17mkj
Politiker Musalia Mudavadi mit seiner Frau Tessie bei einer Pressekonferez, um seine neue Allianz - United Democratic Forum - mit Eugene Wamalwa zu präsentieren. Rechteeinräumung: James Shimanyula räumt der DW ein, dieses Bild unbeschränkt zu nutzen. Bomas of Kenya (in der Nähe von Nairobi)
Mgombea Musalia Mudavadi na mke wakePicha: DW/J. Shimanyula

Mrengo wa Amani unaongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Musalia Mudavadi. Unavishirikisha vyama vya United Democratic Forum (UDF), chama cha KANU kilichong'elewa mamlakani mwongo mmoja uliopita, na pia chama cha New Ford Kenya, chake mwanasiasa chipukizi, Eugene Wamalwa, aliye Waziri wa Sheria.

Mrengo wa amani na maridhiano

Sera za mrengo wa Amani zinalenga katika kuleta amani na maridhiano pamoja na kuimarisha hali ya usalama miongoni mwa wakenya kama anavyopambanua bwana Mudavadi, Kinara wa mrengo huo.

Kulingana na manifesto ya mrengo wa Amani, maswala yanayopewa kipao mbele ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya elimu, swala la kukidhi mahitaji ya chakula na ujenzi wa miundo mbinu kama msingi wa kutimiza malengo ya ruwaza ya mwaka wa 2030.

Shabaha ya kutokomeza ufisadi

Serikali ya muungano wa Amani pia inakusudia kuimarisha mfumo wa ugatuzi, kupambana na ufisadi na kutatua tatizo la ugavi wa mashamba.

Anhänger der neuen Allianz - United Democratic Foreum - von Musalia Mudavadi und Eugene Wamalwa. Rechteeinräumung: James Shimanyula räumt der DW ein, dieses Bild unbeschränkt zu nutzen. Bomas of Kenya (in der Nähe von Nairobi)
Viongozi na wafuasi wa muungano wa AmaniPicha: DW/J. Shimanyula

Bwana Mudavadi, aliye mwana wa aliyekuwa wakati mmoja mwanasiasa mashuhuri katika utawala wa Rais mstaafu Daniel arap Moi, anasema sera zao zipo wazi katika ilani yao. "Ilani yetu haizingatii ahadi za uongo bali inadhamini ujenzi wa taifa, ukuzaji wa uchumi na kuinua hali ya maisha. Ndio, tunatoa ahadi lakini lazima tuzingatie matarajio na hali ilivyo," alisema Mudavadi.

Sifa za mgombea Muadavadi

Viongozi wanaomuunga mkomo bwana Mudavadi wamemminia sifa chungu nzima wakisema kwamba yeye anayo tajriba ya kutosha kuliongoza taifa hili. Bw. Gideon Moi, kiongozi wa chama cha KANU, ambaye pia ni mwanaye Rais mstaafu, Daniel Moi, hakusita kutoa sifa zake kwa kinara huyo wa muungano wa Amani. “Wakati wengine wanachochea taharuki baina ya makabila, Musalia Mudavadi anahimiza uwiano na uaminifu ambapo ukabila ni faida kwani huchangia kuimarisha utamaduni wetu."

Aidha, serikali ya Mudavadi inatoa ahadi kuwa itagharamia masomo kwa wanafunzi wa shule za msingi na za upili. Kadhalika, mrengo huo unaahidi kubuni jumla ya nafasi za kazi milioni mbili kila mwaka, hasa katika sekta ya biashara ndogo ndogo.

Mwandishi: Ruben Kyama
Mhariri: Josephat Charo