1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utambuwe ulimwengu kupitia www.dw.de

5 Februari 2012

Kuanzia Jumatatu ya Februari 6, 2012, Deutsche Welle inajitokeza kwa sura mpya katika mtandao kwa kutumia anuani mpya ya www.dw.de; ruwaza mpya na matangazo ya TV yaliyofanyiwa marekebisho makubwa.

https://p.dw.com/p/13w1O
Deutsche Welle mpya
Deutsche Welle mpya

Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Erik Bettermann, anasema kwamba mabadiliko haya ni hatua muhimu sana katika kuifanya Deutsche Welle “kuwa kioo cha ulimwengu kuiangalia Ujerumani kupitia vyombo vya habari“.

Jukumu letu kama wataalamu wa habari ni kuyaelezea yote yanayotokea ulimwenguni katika upana wake, vipi yanatokezea na athari zake na kuyachambua kwa kina. Mtandao mpya unajumuisha yote yanayotangazwa na DW kupitia njia zote.

dw.de – anwani mpya ya mtandao

Mtandao mpya wa DW unajumuisha yote yanayotangazwa na DW kwa njia ya dijitali: iwe kwa maandishi, vidio, sauti, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi. “Anuani ya dw.de inamaanisha habari za kuaminika kutoka Ujerumani na maelezo yaliyofanunuliwa kwa ujuzi wa hali ya juu wa kiuandishi kwa lugha 30. Mchanganyiko muruwa wa rangi ya kuvutia na ruwaza inayolingana na wakati tulio nao vinaupa mtandao huu sura ya kuvutia," anasema Mkurugenzi Mkuu.

Mkurugenzi Mkuu wa DW, Erik Bettermann
Mkurugenzi Mkuu wa DW, Erik BettermannPicha: DW

Mtandao wa DW unasilisha dhana ya kutegemewa ya mawasiliano yanayozingatia pande zote zinazohusika: mada zilizomo zimepangwa kwa mujibu wa maudhui yake na kadiri ambavyo mtumiaji wa mtandao angezitarajia. Sura ya mtandao huu sasa inatoa fursa kubwa zaidi ya picha, vidio na taarifa za uchambuzi kwa mada mpya katika lugha na njia tofauti.

Ukurasa uliopewa jina la Media Center, ambacho kuanzia sasa ndicho kiini cha utangazaji katika DW, kimeunganishwa na mtandao wa dw.de. Kwa namna hiyo wenye kuutumia mtandao huo wanaweza hapo hapo kuona vidio au picha, kusikiliza matangazo ya redio na kusoma taarifa mbalimbali pamoja na vipindi vyengine kadhaa.

Mada moja, njia nyingi

Kwa mtandao huu mpya na matangazo ya televisheni, Deutsche Welle inaunganisha na kuwasilisha sura mpya. Kawaida mataifa mengi yangelitaka kushiriki katika utoaji wa maoni yao kuhusu ulimwengu na kuufanya umma ushajiike, anasema Mkurugenzi Mkuu. “Kwa muonekano huu mpya wa DW, tunataka kuwekeza katika mafanikio na kuwamo kwenye soko la vyombo vya habari vya kimataifa.“ Hili linajumuisha kutumia majukwaa mapya ya utaalamu na njia za utumaji wa habari unaolingana na dhana hii mpya.

Sura mpya ya Deutsche Welle
Sura mpya ya Deutsche WellePicha: DW

Deutsche Welle imeona mbali kwa kuakisi hali ya wakati ujao na hivyo kutaka kuwa ya kisasa zaidi. Nembo mpya ya Deutsche Welle inawakilisha kazi zote za kiuandishi habari tunazotoa kwa mabara yote, kwa lugha zote, bila ya kujali chombo cha habari kinachohusika, iwe ni redio, televisheni ama mtandao.

Televisheni mpya ya DW

Televisheni ya DW hivi sasa ina chaneli mpya, matangazo mapya na katika muundo mpya. Vipindi vinatoa maelezo kuhusu yale muhimu yanayotokea katika ulimwengu wa habari. Zaidi ya hayo DW itakuwa inatangaza vipindi, usimulizi, ripoti pamoja na kuchambuwa kwa kina masuala mbali mbali.

Lengo la mabadiliko haya ni kuwafikia walengwa wetu popote walipo kwa urahisi, kwa mujibu lugha zao na maeneo yao, ndiyo maana, kwa mfano, kuanzia tarehe 6 Februari 2012, DW itaongeza muda wa matangazo yake ya televisheni kwa Kihispania kwa ajili ya Amerika ya Kusini kuwa masaa 20 kutoka masaa mawili. Kwa Amerika ya Kaskazini, Afrika, Asia na Australia, televisheni ya DW itatangaza kwa masaa 24 kwa siku kwa lugha ya Kiingereza. Maeneo mengine, Amerika ya Kaskazini na Kusini na Asia, televisheni ya DW itakuwa na masaa 20 ya matangazo ya Kijerumani na masaa manne ya Kiingereza. Kwa mataifa ya Kiarabu, masaa 10 kwa Kiarabu na masaa 14 kwa Kiingereza. Kwa Ulaya, masaa 18 kwa Kiingereza na sita kwa Kijerumani.

Nembo mpya ya Deutsche Welle
Nembo mpya ya Deutsche WellePicha: DW

Pamoja na hayo, kuanzia majira ya mapukutiko ya mwaka 2011, makala kuhusu Ulaya kwa lugha za Kiromania, Kikroatia, Kibosnia na Kialbania kwa ajili ya Ulaya ya Kati na Kusini yalianza. Katika idara nyengine, hatua kwa hatua DW inaelekea kwenye kutumia njia nyingi na tofauti za habari.

Muundo mpya wa sauti wa DW

Kwa mara ya kwanza katika historia ya DW kuna kitambulisho cha aina moja tu cha muziki kwa vyombo vyote vya habari. Radio na Televisheni kwa pamoja zina kitambulisho chao ambacho kinamfanya mtu aisikiye hasa ruwaza mpya. Muongozo ni kile kitambulisho cha kituo cha matangazo ambacho mada zake zinaweza kutumiwa kwa aina mbali mbali na redio na televisheni.

Tutumie maoni yako

Je, una masuali au mapendekezo? Tuandikie basi kupitia service@dw.de. Jinsi sura mpya ya DW inavyolingana na pirika pirika zako za maisha, wewe ndie utakayetueleza. Tunafurahi kupokea picha kutoka kila pembe ya dunia na nembo ya DW, naiwe kwa kupiga chapa, kuchora, kuitengeneza kwa mkono, au kufinyanga. Twambieni kwa jinsi gani mnavutiwa na DW. Kwa watakaoshinda miongoni mwa watakaoshiriki kuna zawadi tatu za IPads 2 na simu 20 za Smartphones mpya chapa ya Nokia Lumia 710. Mengi zaidi unaweza kuyapata kupitia: <www.dw.de/mydw>.

Mwandishi: Birgit Görtz
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Andrea Schmidt