1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Utandawazi kwa njia mbadala"

Maja Dreyer5 Juni 2007

Akiwa ni mgeni wa kwanza wa mkutano wa kilele wa nchi nane zinazoongoza kiviwanda duniani G8, leo hii Rais Bush atawasili Ujerumani. Kesho atakutana pamoja na wenzake viongozi saba wengine mjini Heiligendamm, Kaskazini mwa Ujerumani, pamoja na wageni wa nchi nyingine kama vile China, India au Afrika Kusini. Wakati huo huo, mjini Rostock ambao ni karibu na Heiligendamm kuna mkutano mwingine ambao ni kama mkusanyiko wa wapinzani wa sera za utandawazi.

https://p.dw.com/p/CHD7
Watu wengi wanapinga sera za utandawazi
Watu wengi wanapinga sera za utandawaziPicha: AP

Chini ya maneno makuu: Utandawazi kwa njia mbadala”, wajumbe elfu moja kutokana duniani kote wanakutana wiki hii mjini Rostock kuanzia leo hadi Alhamisi. Lengo lao ni kuweka wazi mawazo mapya ambayo ni tofauti kuliko sera za nchi tajiri. Masuala muhimu kwenye mkutano huu ni ulinzi wa hali ya hewa na vita dhidi ya maskini. Akifungua rasmi mkutano huu, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa anayearifu juu ya kupatikana chakula duniani, Jan Ziegler, alizikosoa vikali nchi za Umoja wa Ulaya kwa kuathiri uchumi katika nchi maskini kwa sera zao za ruzuku.

Bw. Ziegler alisema: "Ninakupa mfano mmoja tu. Barani Afrika, siku hizi, kwenye kila soko unaweza kupata mboga kutoka Ujerumani, Italy au Ufaransa kwa bei ambayo ni nusu au theluthi moja ya bei za mboga za kienyeji. Sababu ni kwamba Umoja wa Ulaya umelipa mabillioni ya Euro kama ruzuku ili mazao yauzwe nje ya Ulaya. Hiyo ni sera mbaya sana ambayo inawaua mamia ya watu kila siku. Na hiyo inaweza kusimamishwa leo na sasa hivi.”

Waandalizi wa mkutano wa Rostock ni ushirikiano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanapungua 40, yakiwemo pia mashirika ya kimataifa kama vile Oxfam na Greenpeace.

Karsten Smid wa shirika la Greenpeace, linalopigania ulinzi wa mazingira, alitoa mwito kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye anaongoza mkutano wa kundi la G8 kubeba jukumu muhimu katika kulinda hali ya hewa. Kinachohitajika ni masharti ya kupunguza utoaji wa gesi chafu badala ya porojo tu, alisema Bw. Smid.

Jan Ziegler wa Umoja wa Mataifa pia alilalamikia maslahi ya kiuchumi ya nchi za Magharibi. Yale ambayo yanapewa umuhimu ni usalama wa kuwekeza kiuchumi. Njaa haizungumziwi miongoni mwa wanasiasa hao.

Jan Ziegler: “Mimi natoka Nigeria sasa hivi. Rais Umaru Yar'Adua ambaye alichaguliwa kwa njia isiyo halali, ni mgeni rasmi wa mkutano wa G8. Lakini nchini Nigeria kuna balaa kubwa, kuna njaa, magonjwa yanaenea, kuna watu wengi wasioweza kusoma wala kuandika, hata hivyo ni nchi inayochukua nafasi ya tano kati ya watoaji mafuta duniani. Mimi nadhani si sawa ikiwa nchi na Magharibi zinashirikiana na Wanigeria, kwa mfano kwa kuwekeza kiuchumi bila ya watu wa kawaida kunufaika.”

Jane Nalunga wa shirika la “Seatini” kutoka Uganda alidai msaada unaotolewa Afrika uwe bora zaidi na bila ya masharti. Bara la Afrika linahitaji mfumo wa biashara duniani ulio sawa, alisema Bi Nalunga.