1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa hali ya hatari Ufaransa washutumiwa

Admin.WagnerD4 Februari 2016

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu Amnesty limeshutumu utawala wa hali ya hatari Ufaransa na umeitaka serikali kutorefusha muda wa utawala huo.

https://p.dw.com/p/1HpeU
Polisi katika doria karibu na Mnara wa Paris.
Polisi katika doria karibu na Mnara wa Paris.Picha: picture-alliance/dpa/G. Horcajuelo

Shirika la Amnesty International limehoji nguvu inayotumika katika utekelezaji wa utawala wa hali ya hatari nchini Ufaransa. Kiongozi wa tawi la Amnesty barani Ulaya John Dalhusein ameonya katika taarifa ya utafiti wa shirika hilo iliochapishwa Alhamisi (04.01.2015) " Iwapo serikali inaweza kuchukuwa hatua maalum katika mazingira maalum basi lazima ifanye hivyo kwa tahadhari."

Amnesty imetathmini matokeo ya wale walioathirika kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya mwezi Novemba mjini Paris. Dalhusein amesema "Uhalisia wa kile tulichokishuhudia Ufaransa ni kwamba madaraka makubwa ya utendaji yaliyotolewa kwa polisi na waendesha mashtaka yamesababisha ukiukaji kadhaa wa haki za binaadamu."

Amnesty inasema misako ya usiku inapelekea kunyanyapaliwa na kuparaganyika kiakili kwa wahusika.Takriban watu sitini walipoteza ajira zao kufuatia misako hiyo.Kwa mujibu wa shirika hilo kumekuwepo na misako ya nyumba 3000 na zaidi ya vifungo vya nyumbani 400 tokea kuzuka kwa mashambulizi hayo ya kigaidi.

Hali ya hatari sio suluhisho

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International lenye makao yake mjini London Uingereza linasisitiza kwamba utawala wa hali ya hatari hauwezi kuwa suluhisho la kudumu bila ya kuathiri uhuru wa msingi.

Kumbukumbu ya mashambulizi ya kigaidi Paris.
Kumbukumbu ya mashambulizi ya kigaidi Paris.Picha: DW/E. Serwettaz

Tawi la Amnesty International mjini Paris limesema katika taarifa leo hii kwamba hatua ambazo zimo kwenye mpango huo wa utawala wa hali ya hatari ikiwa ni pamoja na misako ya nyumba wakati wa usiku bila ya kibali cha mahakama,marufuku ya mikusanyiko ya watu na kifungo cha nyumbani kwa mtuhumiwa wa ugaidi hayawezi kuleta tija madhubuti.Imesema badala yake itawanyanyapaa watu na imewapotezea baadhi ya watu ajira zao.

Uamuzi wa serikali ya Ufaransa hapo jana kutaka kuongezewa muda wa miezi mitatu kwa utawala wa hali ya hatari ambao ulitangazwa nchini humo baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliouwa watu 130 mjini Paris hapo mwezi Novemba unashutumiwa na mashirika ya haki za binaadamu kwa kuvuruga demokrasia.Ombi hilo lililopendekezwa jana katika mkutano wa baraza la mawaziri sasa linahitaji idhini ya bunge.

Tishio kwa uhuru wa kiraia

Mageuzi tata ya kisheria kuhusiana na mpango huo wa utawala wa hali ya hatari unaimarisha madaraka ya polisi na waendesha mashtaka sawa na yale yanayotakiwa kutumika wakati wa hali ya hatari.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa (kulia) na Waziri Mkuu Manuel Valls.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa (kulia) na Waziri Mkuu Manuel Valls.Picha: picture-alliance/abaca

Wakosoaji wanaona mageuzi hayo ya sheria ni tishio kwa uhuru wa kiraia na wanashutumu kwamba dhima ya jaji wa kujitegemea wa masuala ya uchunguzi itadhoofishwa.

Utawala wa hali ya hatari muda wake tayari umeongezewa mara moja na ulikuwa umalizike Februari 26. Katika taarifa ya maandishi Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema kuongezewa muda wa miezi mitatu kunahalalishwa kutokana na haja ilioko ya kukabiliana na tishio la ugaidi.

Kuuwa watuhumiwa wa ugaidi

Muswada mwengine wa serikali ambao uliowasilishwa hapo jana unawapa polisi ruhusa ya kutumia silaha zao kumdhibiti mtu ambaye ndio kwanza ameuwa au kufanya mauaji kadhaa na yumkini mtu huyo akarudia uhalifu huo.

Ali Salah mmojawapo ya washambuliaji katika mashambulizi ya Paris aliyeuwawa.
Ali Salah mmojawapo ya washambuliaji katika mashambulizi ya Paris aliyeuwawa.Picha: Polizei NRW

Kwa sasa ni kutumia silaha kwa kujihami tu ndio halali kisheria kumpiga mtu risasi.

Makundi kadhaa ya haki za binaadamu yanapinga kuongezewa muda kwa utawala wa hali ya hatari na maelfu ya watu waliandamana mjini Paris hapo Jumapili kupinga hilo.

Chama cha haki za binaadamu nchini Ufaransa kimesema katika taarifa ya maandishi kwamba hawapaswi kuziachia haki zao na uhuru wao.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Daniel Gakuba