1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

Utawala wa Kijeshi wa Myanmar wapunguza kifungo cha Suu Kyi

1 Agosti 2023

Utawala wa kijeshi nchini Myanmar umetangaza hatua ya msamaha wa jumla kwa wafungwa na kusema itapunguza muda wa kifungo kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Aung San Suu Kyi.

https://p.dw.com/p/4UdVt
Myanmar Aung San Suu Kyi
Picha: Nyein Chan Naing/AP/picture alliance

Vyombo vya habari vya serikali ya Myanmar vimeripoti leo Jumanne kuwa Rais wa zamani Win Myint na Suu Kyi, mwenye umri wa miaka 78, watapokea nusu ya msamaha inayomaanisha kuwa muda wao wa vifungo utapunguzwa.

Utawala wa kijeshi wa Myanmar umetoa msamaha huo kwa kiongozi wa zamani Aung San Suu Kyi kwa kumsamehe makosa matano kati ya 19 ambayo alihukumiwa lakini wakasisitiza kuwa atasalia kwenye kifungo cha nyumbani .

Soma pia: Utawala wa kijeshi wa Myanmar warefusha muda hali ya dharura

Makosa ambayo Suu Kyi amesamehewa ni madogo ikiwa ni pamoja na kukiuka sheria ya kukabiliana na maafa ya asili kuhusu sheria za kupambana na janga la UVIKO-19 wakati wa kampeni zake. Tovuti ya habari ya "Myanmar Today" imeripoti kwamba viongozi hao wa zamani hawatopewa msamaha kamili na watasalia vifungoni.

Myanmar Naypidaw | Win Myint und Aung San Suu Kyi
Myanmar: Kiongozi wa zamani Aung San Suu Kyi (kulia) akiwa na rais wa zamani Win MyintPicha: That Aung/AFP/Getty Images

Msemaji wa utawala wa kijeshi nchini Myanmar Zaw Min Tun ameliambia shirika la habari la Eleven Media Group kwamba msamaha huo unamaanisha kuwa miaka sita ya kifungo itaondolewa kwa Suu Kyi aliyehukumiwa miaka 33 jela na kuongeza kuwa ilikuwa ni sehemu ya msamaha wa jumla ambapo zaidi ya wafungwa 7,000 waliachiliwa kote katika nchi hiyo yenye migogoro.

Soma pia: Indonesia yahimiza suluhisho la kisiasa Myanmar

Baada ya mapinduzi ya Februari 1, 2021, jeshi lilimuondoa madarakani na kumuwekwa kizuizini mkuu wa serikali aliyechaguliwa kidemokrasia Suu Kyi. Baadaye, Mahakama inayodhibitiwa na Jeshi ilimhukumu Suu Kyi zaidi ya miaka 30 jela kwa  makosa kadhaa ya uhalifu.

Mshindi huyo wa Tuzo ya amani ya Nobel alihamishwa wiki iliyopita kutoka jela na sasa anatumikia kifungo cha nyumbani katika mji mkuu, Naypyitaw. Suu Kyi anakanusha na maekuwa akikata rufaa kwa mashtaka yote yaliyomtia hatiani ikiwa ni pamoja na uchochezi, udanganyifu katika uchaguzi pamoja na rushwa.

Rais wa zamani apunguziwa pia kifungo

Myanmar | Min Aung Hlaing
Kiongozi wa Kijeshi wa Myanmar Jenerali Min Aung HlaingPicha: The Military True News Information Team via AP/picture alliance

Win Myint pia alikuwa miongoni mwa waliohukumiwa kwenda jela kwa miaka mingi. Msemaji wa utawala wa kijeshi huko Myanmar alinukuliwa akisema kuwa Win Myint ambaye alikamatwa wakati mmoja na Suu Kyi, amepunguziwa pia miaka minne katika kifungo chake.

Soma pia: UN: Wafanyakazi 40 wa misaada waliuawa nchini Myanmar tangu mapinduzi ya 2021

Siku ya Jumatatu, jeshi liliahirisha uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu na badala yake likaongeza muda wa hali ya dharura kwa miezi sita zaidi, jambo ambalo wakosoaji wanasema linaweza kuchochea mzozo uliopo.

Chama cha Suu Kyi kilishinda uchaguzi wa Novemba mwaka 2020 lakini jeshi la Myanmar lilitaja kuwepo kwa udanganyifu na kuchukua madaraka mwaka 2021 likidai kuanzisha na kusimia uchunguzi wa madai hayo. Chama cha Suu Kyi kilitupilia mbali tuhuma hizo za udanganyifu katika uchaguzi wa Myanmar.