1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Marekani wabadilisha mbinu kuelekea mataifa mengine.

Sekione Kitojo5 Mei 2007

Ikiwa na muda wa miezi 18 tu hadi kumaliza kipindi cha madaraka yake , utawala wa rais George W. Bush nchini Marekani unaonekana kwa mara nyingine tena kuelekea katika mtazamo halisi katika kushughulika na mataifa mengine duniani , ikiwa ni pamoja na mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/CHEo
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani katika mkutano na waandishi wa habari katika mji wa Sham el Sheikh Misr baada ya mkutano na viongozi wengine.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani katika mkutano na waandishi wa habari katika mji wa Sham el Sheikh Misr baada ya mkutano na viongozi wengine.Picha: AP

Ishara kubwa kabisa imekuja wakati wa mkutano wa wiki iliyopita wa kimkoa katika mji wa kitalii nchini Misr wa Sham el-Sheikh, ambapo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice alitumia dakika 30 kwa mazungumzo ya ana kwa ana na waziri mwenzake wa Syria , Walid al-Moallem , katika mazungumzo yanayosemekana kuwa yalilenga katika kutafuta kupatikana kwa ushirikiano wa muda mrefu kutoka Damascus na kufunga mipaka yake na Iraq.

Ulikuwa mkutano wa kwanza baina ya mataifa hayo katika ngazi ya mawaziri tangu kuuwawa mwezi Februari 2005 kwa waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri , ambapo Marekani ilimrejesha balozi wake kutoka Damascus wakipinga hatua hiyo.

Wakati Rice baadaye alisisitiza kuwa mkutano wake ulikuwa tofauti na ziara iliyokuwa na utata ya spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi kutoka chama cha Democratic kwasababu majadiliano yalihusika tu na Iraq na hakuna mpiga picha aliyekuwapo katika mkutano huo , wachunguzi wengi wa masuala ya kisiasa wanauona mkutano huo kuwa muhimu sana katika hatua za kuelekea katika utekelezaji wa mapendekezo muhimu ya kundi lililofanya uchunguzi kuhusu hali ya Iraq, ISG kundi lililokuwa chini ya uenyekiti wa James Baker.

Ghafla mkutano na serikali ya Syria sio tena tukio la uhaini mkubwa, ameandika Juan Cole, mtaalamu wa masuala ya mashariki ya kati katika chuo kikuu cha Michigan katika tovuti yake maarufu, na kudokeza kuwa Rice alitaka pia ushauri kutoka kwa Pelosi kabla ya kuanza safari yake.

Naweza tu kufikiri kuwa mkutano wa Condi na Mouallem ni ishara kuwa nguvu za makamu wa rais Dick Cheney madarakani ndani ya Ikulu ya Marekani zinaanza kupungua sana, na kwamba Condi anasikilizwa zaidi na Bush juu ya haja ya kuzungumza.

Cheney , kiongozi wa wapenda vita katika utawala wa rais Bush , ameshutumu hadharani ziara ya Pelosi mjini Damascus kuwa ni tabia mbaya, wakati baadhi ya washirika wake wahafidhina mamboleo nje ya utawala huo walitaka hata ashitakiwe mahakamani chini ya sheria iliyodumu kwa muda wa miaka 200 ambayo inafanya kuwa ni uhalifu kwa mtu raia wa nchi hiyo kuwasiliana na serikali ya nje ambayo ni adui ili kushawishi tabia zao.

Cheney ambaye bado anaomboleza kutokana na kukubali kwa Bush, kufuatia ombi la binafsi la Rice katika makubaliano ya kinuklia na Korea ya kaskazini February mwaka huu, amepata pigo jingine wiki hii wakati Ikulu ya Marekani ilipotangaza kujiuzulu kwa naibu mshauri wa masuala ya kiusalama wa taifa J.D. Crouch, mtu mwenye msimamo mkali ambaye alikuwa anashughulikia masuala ya kila siku ya baraza la taifa la usalama NSC katika wakati wa awamu ya pili ya utawala wa rais Bush.

Hali hiyo ni mbaya kwa wapenda vita katika utawala wa rais Bush ambao wamekuwa wakiona idadi yao ikipungua kila wakati tangu kuanza kwa kipindi cha pili cha utawala wa rais Bush.

Walianza kupoteza ngome yao kuu katika wizara ya ulinzi kwa kuondoka kwa Wolfowitz mwaka 2005 na mhafidhina mamboleo , naibu waziri wa sera Douglas Feith. Kuondoka Novemba mwaka jana kwa Donald Rumsfeld na wadhifa wake kuchukuliwa na Robert Gates , mtu ambaye anaangalia mambo kwa uhalisi wake na mtu wa karibu wa james Baker katika wizara ya ulinzi , kulimpoteza kwa mara nyingine tena mshirika mwingine mkubwa wa Cheney, wakati naibu waziri katika wizara ya ulinzi chini ya Rumsfeld aliyekuwa anashughilikia masuala ya taarifa za kijasusi, Stephen Cambone, na waziri mdogo wa masuala ya usalama wa kimataifa Peter Rodman, wote wamepumzishwa.