1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Syria wapoteza uhalali - EU

Mohamed Dahman11 Mei 2011

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema utawala wa Syria umepoteza uhalali wake huku Umoja huo ukimshinikiza Rais Bashar Al Assad kwa kumuonya kwamba vikwazo vinaweza pia kuwekwa dhidi yake.

https://p.dw.com/p/11Day
Bashar al-Assad, kaka yake Maher, na shemegi yake Assef Shawkat
Bashar al-Assad, kaka yake Maher, na shemegi yake Assef ShawkatPicha: AP

Umoja wa Ulaya hapo jana umemuweka kaka mdogo wa Rais Assad, Maher al Assad, mwenye umri wa miaka 43, kwenye orodha ya maafisa waandamizi 13 ambao mali zao zitazuiliwa na pamoja na kuwekewa marufuku ya viza za kuingia Ulaya, ikiwa ni sehemu ya hatua kadhaa zenye kujumuisha vikwazo vya silaha na zana zinazotumika kwa ajili ya kuwakandamiza wananchi wake. Mabinamu wanne wa rais pia wamo kwenye orodha hiyo.

Watu hao 13 waliomo kwenye orodha hiyo ni pamoja na Mkuu wa Ujasusi, Ali Mamluk, na waziri mpya wa mambo ya ndani, Mohammed Ibrahim al-Shaar, ambao wamehusishwa na ukatili dhidi ya waandamanaji.

Akilihutubia bunge la Umoja wa Ulaya mjini Strassbourg leo hii, Mkuu wa Sera za Kigeni wa umoja huo, Catherine Ashton, amesema Syria imepoteza uhali wa utawala wake na imeutaka utawale huo ubadili mwelekeo wake.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine AshtonPicha: AP

Ashton amesema kinachojiri Syria ni kilio cha umma unaodai demokrasia na utawala wa sheria na sio njama kutoka nje na kwamba kushindwa kutambuwa kinachojiri nchini humo serikali inapoteza uhalali wake na inajitenga na wananchi wake halikadhalika jumuiya ya kimataifa.

Umoja wa Ulaya ambao umegawika juu ya hatua gani ya kuchukuwa kukomesha ukandamzaji wa Syria kwa waandamanaji umemwacha Assad katika vikwazo hivyo, wakati ikimuonya iwapo atashindwa kubadili sera zake yeye pia anaweza kuchukuliwa hatua ya kuadhibwa.

Katika taarifa iliotolewa wakati vikwazo hivyo vikianza kufanya kazi, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema hatua hizo zinakusudia kuyafanya yafanikiwe mabadiliko ya haraka ya sera,kukomesha mkondo wa ukatili na kuanzisha mara moja mageuzi ya dhati ya kisiasa.

Amesema kushindwa kufanya hayo Umoja wa Ulaya itafikiria kuchukuwa hatua, zikiwemo za kuuwekea vikwazo uongozi wa juu.

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi la nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya wataliangalia upya suala hilo katika mazungumzo yaliopangwa kufanyika hapo tarehe 23 mwezi huu wa Mei.

Mjini Berlin Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ameionya Syria kwamba itakabiliwa na hatua kali zaidi ya Umoja wa Ulaya iwapo haitokomesha ukatili dhidi ya raia wake.

Amesema vikwazo hivyo vilivyowekwa ni hatua ya mwanzo, na iwapo serikali ya Syria itaendelea na ukandamizaji wake wataongeza shinikizo lao.

Vikosi vya Syria vimeendelea kuizingira miji mikuu iliozuka machafuko, ukiwemo wa Banias na kuvifunga vitongoji vya karibu pamoja na kuwakamata viongozi wa upinzani.

Vifaru ya jeshi la Syria leo vimeushambulia mji wa Holms uliojichomoza kuwa wa tatu kwa ukubwa kwa kuwa na upinzani mkali dhidi ya utawala wa Syria.

Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu watu kati ya 600 hadi 700 wameuwawa na takriban 800 wamekamatwa tokea kuanza kwa vuguvugu la maandamano dhidi ya serikali katikati ya mwezi wa Machi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ RTR/AFP

Mhariri: Miraji Othman