1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utulivu Syria huku maeneo mengine yakiripotiwa mapigano

MjahidA26 Oktoba 2012

Shirika la televisheni la Syria leo asubuhi limemuonesha rais wa nchi hiyo Bashar Al Assad, akihudhuria sala ya Idd ul Adha.

https://p.dw.com/p/16XY2
Rais Bashar Al Assad kwenye Sala ya Idd ul Adha
Rais Bashar Al Assad kwenye Sala ya Idd ul AdhaPicha: Reuters

Hata hivyo licha ya utawala wa nchi hiyo kutangaza kusitisha mapigano, katika siku nne ya kusherehekea siku hii kuu kwa waumini wa kiislamu, bado kuna habari za kuendelea kwa mapigano .

Bashar Al Assad akionekana kuwa mtulivu na mwenye tabasamu kubwa alihudhuria sala ya asubuhi ya Idd ul Adha katika msikiti mmoja mjini Damascus. Hii leo pande zote mbili, serikali na makundi kadhaa ya waasi yalikubaliana kusitisha mapigano kuanzia leo asubuhi hadi siku ya jumatatu. Akitoa hotuba yake Imamu wa msikiti huo Walid Abdel Haq alitaka wasyria kuwacha kuzozana kwa kuwa wote ni ndugu moja.

Imam Walid amesema mapigano na mauaji yameendelea kwa miaka miwili nchini humo na ni lazima jambo hilo likomeshwe. Baada ya Sala hiyo Rais Assad alionekana akisalimiana na waumini wengine huku akizungumza nao kwa furaha.

Maandamano Syria

Maandamano ya kumpinga Rais Bashar Al Assad.
Maandamano ya kumpinga Rais Bashar Al Assad.Picha: Reuters

Hata hivyo licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano katika siku nne za kusherehekea Idd ul Adha, maandamano ya kupinga utawala wa rais Bashar yalifanyika. Hii ni kulingana na wanaharakati nchini humo pamoja na mashirika ya kutetea haki za binaadamu. Maandamano hayo yametokea wakati kukiwa kutulivu nchini Syria baada ya makubaliano ya kusitisha vurugu.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu nchini Syria, kumekuwa na mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasi karibu na kambi moja ya kijeshi kaskazini mwa mji wa Maaret al-Numan. Shirika hilo limesema maandamano yametokea katika eneo moja la Raqa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambapo vikosi vya serikali vimeripotiwa kurusha mabomu ya kutoa machozi. Watu watatu wameripotiwa pia kujeruhiwa Katika eneo la Daraa kusini mwa nchi hiyo baada ya polisi kufvyatua risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji.

Nako mjini Idlib waandamanaji walisema kwa sauti, Ondoka rais Assad wewe ni msaliti umeiharibu Syria. Hata hivyo upinzani ulitumia mtandao wa kijamii facebook kuwataka watu nchini Syria waandamane, wakisema hatua ya kusimamishwa mapigano ni nafasi kwao kuandamana kwa nguvu zote.

Mjumbe wa upatanishi Syria Lakhdar Brahimi
Mjumbe wa upatanishi Syria Lakhdar BrahimiPicha: Reuters

Kulingana na sheria za Syria ni kinyume cha sheria kufanya maandamano ya aina yoyote yale bila kupata kibali cha serikali.

Mpango wa kusimamisha mapigano ulizingatiwa baada ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa na hata jumuiya ya nchi za kiarabu kwa ajili ya Syria Lakhdar Brahimi, kupendekeza hilo kwa pande zote mbili ili kutoa nafasi kwa waislamu wa Syria kusherehekea iidi yao kwa amani. Tangu kuanza kwa mapigano takriban miezi 20 iliopita watu zaidi ya 30,000 wameuwawa na wengine wengi kupoteza makaazi yao.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman