1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya mwisho yanatarajiwa kukamilishwa karibuni

Mjahida 8 Aprili 2016

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imesema hatua zimepigwa katika mazungumzo na Israel yaliyofanyika wiki hii, kuhusu kerejesha mahusiano baina ya nchi hizo mbili yaliyoyumba kutokana na hali katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/1ISE1
Türkei Recep Tayyip Erdogan in Ankara
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/Presidential Press Office

Kulingana na taarifa ya Wizara ya mambo ya nje ya Uturuiki, mpango huo unatarajiwa kukamilishwa katika mkutano utakaofanyika hivi karibuni. Kwa upande wake gazeti la Haaretz la Israel limeripoti kuwa, mazungumzo yaliyofanyika jijini London na kuwakilishwa na ujumbe kutoka kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu na afisa mkuu wa wizara ya kigeni ya Uturuki ulifanyika vizuri na kukamilika siku ya alhamisi ( 07. 04. 2016 )

Hata hivyo mwanya uliyowachwa wazi katika mazungumzo hayo ni matakwa ya Uturuki ya kuitaka Isarel iache kuizingira Palestina katika eneo linalopiganiwa la ukanda wa Gaza huku Isarel nayo ikisisitiza kuwa Uturuki, ifungie operesheni za wanamgambo wa Hamas mjini Istanbul.

Israel Benjamin Netanjahu Fahne
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Balilty

Hatua ya kuizingira Gaza imeelezewa na makundi ya kutetea haki za binaadamu kama ya kikatili na isiyokuwa ya kibinaadamu, ijapokuwa Israel imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuzuwiya biashara haramu ya silaha.

Huku hayo yakiarifiwa maafisa wa Uturiki na chombo cha habari cha serikali nchini Uturuki wamekuwa na maono chanya juu ya maridhiano na Israel. Rais Recep Tayyip Erdogan wiki moja iliyopita alikutana na makundi ya wayahudi akiwa ziarani nchini Marekani, kujadili namna ya kukabiliana na ugaidi na suala la ubaguzi.

Marekani yazihimiza Uturuki na Isarel kupatana

Uturuki ilikasirishwa na hatua ya Israel ya kulishambulia eneo la Gaza mapema mwaka wa 2009. Mwaka unaofuata raia takriban 10 wa Uturuki waliuwawa wakati wanajeshi wa majini kutoka Israel walipoivamia boti la misaada lililokuwa linaelekea Gaza na kusababisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili kuanza kuyumba.

Mwaka wa 2013, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akaelezea masikitiko yake juu ya vifo hivyo huku utawala wa Marekani ukizihimiza nchi hizo mbili kupatana.

Treffen von John Kerry mit Tayyip Erdogan
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na rais wa Uturiki wa Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/Anadolu Agency/K. Ozer

Lakini mwaka wa 2014 wakati wa mapigano ya Israel na wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza, rais Erdogan alivikosoa vikali vikosi vya Isarel na kuvishutumu kutekeleza mauaji ya halaiki na kuwa na ukatili zaidi kuliko kiongozi wa wanazi Adolf Hitler.

Aidha wachambuzi wanasema muelekeo wa Uturuki umechangiwa na mahusiano mabaya kati yake na Urusi tangu kudunguliwa kwa ndege ya Urusi na Uturuki hali iliyochangia miradi kadhaa ya pamoja kufutiliwa mbali. Uturuki inaitegemea Urusi kwa zaidi ya nusu ya gesi na kwa sasa nchi hiyo inaangalia hifadhi ya gesi ya Israel.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga