1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yadungua ndege ya kijeshi ya Urusi

Grace Kabogo24 Novemba 2015

Rais wa Urusi, Vladmir Putin, amesema kitendo cha Uturuki kuidungua ndege yake ya kivita mpakani mwa Syria, ni sawa na kuchomwa kisu mgongoni na kwamba ndege hiyo haikuwa na kitisho chochote kwa Uturuki.

https://p.dw.com/p/1HBtQ
Ndege ya kijeshi ya Urusi
Picha: picture-alliance/dpa/Anadolu Agency

Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema kitendo cha Uturuki kuidungua ndege yake ya kivita mpakani mwa Syria, ni sawa na kuchomwa kisu mgongoni na kwamba ndege hiyo haikuwa na kitisho chochote kwa Uturuki.

Akizungumza mjini Sochi, wakati wa mkutano wake na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan, Putin amesema kitendo hicho kitakuwa na madhara makubwa katika uhusiano wa Urusi na Uturuki. Amesema watakitathmini kitendo hicho kubaini yale yote yaliyotokea. Amefafanua kuwa kitendo cha Uturuki kuidungua ndege yake ya kivita chapa SU-24, kimefanywa na washirika wa magaidi.

Amekanusha taarifa kwamba ndege hiyo ambayo Uturuki inadai ilipuuza onyo walilolitoa, ilivuka mpaka wa Syria na kuingia katika anga ya Uturuki bila ya idhini, akisema imeangukia umbali wa kilomita 4 kutoka kwenye mpaka wa Uturuki.

''Ndege yetu ilidunguliwa katika ardhi ya Syria kwa kombora lililorushwa na ndege za kijeshi za Uturuki chapa F-16. Wakati iliposhambuliwa ilikuwa angani umbali wa futi 19,685, ambayo ni kilomita 1 kutoka kwenye mpaka na Uturuki. Hivyo haikuwa na kitisho chochote kwa jamhuri ya Uturuki,'' alisema Putin.

Putin aikosoa Uturuki

Rais Putin pia ameikosoa hatua ya Uturuki kuigeukia Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuzungumzia tukio hilo, badala ya kwanza kuelezea kile kilichotokea kwa Urusi na ametoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha rubani wa Urusi ambaye iliripotiwa kwamba alitekwa nyara na kisha kuuawa.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema atachukua hatua dhidi ya waliodungua ndege
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema atachukua hatua dhidi ya waliodungua ndegePicha: picture-alliance/AP Photo/A. Nikolsky

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu amesema leo kuwa nchi yake ilikuwa na haki ya kimataifa na wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya mtu anayekiuka anga au mipaka yake. Akizungumza kwenye mji mkuu wa Uturuki, Ankara, Davutoglu, amesema dunia inapaswa kufahamu kwamba Uturuki itafanya chochote kinachowezekana kwa ajili ya usalama wa nchi hiyo.

Wakati hayo yanajiri, wizara ya mambo ya nje ya Uturuki leo imewaita wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao ni Marekani, Urusi, Ufaransa, China na Uingereza, ili kuwaeleza kuhusu kilichosababisha waidungue ndege ya kivita ya Urusi.

Wakati huo huo mabalozi wa NATO watakutana kwa dharura, mkutano unaofanyika kutokana na ombi la Uturuki, baada ya nchi hiyo kuidungua ndege ya kivita ya Urusi. Mkutano huo wa Baraza linalopitisha maamuzi ndani ya NATO na kuwajumuisha mabalozi kutoka Marekani na nchi nyingine 27 wanachama wa NATO, utafanyika jioni hii, ambapo Uturuki itawaeleza washirika wake kuhusu kudunguliwa kwa ndege hiyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu