1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege hiyo iliingia katika anga yake Syria

16 Oktoba 2015

Jeshi la Uturuki limedai kuwa ndege zake za kijeshi zimeidungua ndege isiyo na rubani, ambayo iliingia katika anga ya Uturuki karibu na mpaka wake na Syria.

https://p.dw.com/p/1GpUD
Ndege isiyo na rubani, chapa MQ-9
Ndege isiyo na rubani, chapa MQ-9Picha: picture-alliance/AP/Air Force/L. Pratt

Duru za kijeshi zimeeleza kuwa ndege hiyo imedunguliwa leo baada ya kukiuka tahadhari na kuonywa mara tatu ili iweze kuondoka, baada ya kuingia ndani ya eneo la anga la Syria.

Hata hivyo, haikufahamika mara moja ndege hiyo iliyoangukia ndani ya mipaka ya Uturuki, ni ya nchi gani. Ndege hiyo imeangukia kwenye eneo la Kilis, lililoko umbali wa kilomita 90 na mji wa kaskazini mwa Syria, Aleppo.

Urusi ambayo inafanya mashambulizi ya anga nchini Syria, imesema kwa upande wake ndege zake zote za kivita nchini Syria zimerejea kwenye kambi na kwamba ndege zake za upelelezi ambazo hazina rubani, zinaendesha shughuli zake kama kawaida.

Msemaji wa wizara hiyo, Jenerali Igor Konashenkov, amesema leo kuwa ndege zote za jeshi la Urusi zilizoko kwenye Jamhuri ya Syria, zimerejea kwenye kambi ya kijeshi ya Humaymim, baada ya kukamilisha operesheni za kijeshi.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu
Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet DavutogluPicha: Reuters/Umit Bektas

Serikali za Marekani, Urusi na Syria zote zinazo ndege zisizo na rubani ambazo ziko katika ukanda huo. Hata hivyo, hapajakuwa na maelezo ya haraka yaliyotolewa kuhusu ndege hiyo isiyo na rubani kutoka kwenye ubalozi wa Marekani nchini Uturuki.

Uturuki ilitoa onyo

Mwanzoni mwa mwezi huu, Uturuki ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, iliionya Urusi mara mbili kutokana na ukiukwaji unaofanywa na ndege zake za kivita kwenye anga yake.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu alionya kuwa nchi yake itabadilisha sheria zake za kijeshi bila kujali ni nani anakiuka matumizi ya anga yake na kwamba vikosi vyenye silaha tayari vimeshapewa maelekezo.

Urusi ilianza operesheni ya kupambana na kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS na makundi mengine ya wanamgambo nchini Syria, mwishoni mwa mwezi uliopita katika juhudi za kuiunga mkono serikali ya Syria, ambayo ni mshirika mkuu wa Urusi katika Mashariki ya Kati.

Tangu mwaka 2013, Uturuki imeidungua ndege ya kijeshi ya Syria, helikopta na ndege isiyo na rubani, ambayo ilipotea katika anga ya Uturuki. Matukio hayo yalitokea baada ya kufanyia mabadiliko sheria zake za ushiriki wake kutokana na Syria kuidungua ndege ya kijeshi ya Uturuki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,DPAE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman