1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaionya Iran juu ya Syria

8 Agosti 2012

Kila upande unadai kuudhibiti wa mji wa Aleppo, huku mapigano makali yakiendelea kati ya serikali na waasi na Uturuki ikiionya Iran kwa kuihusisha na ghasia za Syria, nayo Iran yenyewe ikiitisha mkutano juu ya Syria.

https://p.dw.com/p/15luF
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmed Davotuglu.

Shirika la habari la serikali, SANA, limesema wanajeshi wa serikali wamechukuwa udhibiti wa wilaya ya Salaheddine, baada ya kusababisha hasara na madhara makubwa kwa upande wa wale lililowaita "magaidi wenye silaha". Kwa mujibu wa shirika hilo, waasi wengi wameuawa, kujeruhiwa na wengine kukamatwa mateka. Aidha jeshi la serikali limekamata idadi kubwa ya silaha zilizokuwa mikononi mwa waasi.

Hata hivyo, upande wa waasi umekanusha kutwaliwa kwa wilaya ya Salaheddine, ingawa umekiri kufanyika kile walichokiita "mashambulizi makali na ya kikatili" kutoka kwa jeshi la serikali katika wilaya ya hiyo ambayo imekuwa ikishikiliwa na waasi kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

Kanali Abdel Jabbar al-Oqaidi wa Jeshi Huru la Syria amesema jeshi la serikali linatumia kila silaha na mbinu kuishambulia wilaya hiyo, vikiwemo vifaru, ndege na makombora, lakini bado imo mikononi mwao.

Kanali Oqaidi amesema mapigano yanaendelea pia kwenye wilaya nyengine nyingi, ingawa pande zote mbili zimejikita kwenye wilaya ya Salahiddine kwa sababu ya umuhimu wake.

Afisa mmoja wa usalama wa serikali, amenukuliwa akisema kwamba mapambano ya kuwamaliza waasi waliobakia yataendelea hadi asubuhi ya kesho, kwani lengo la jeshi ni kuichukua pia wilaya ya Seif al-Dawla, iliyo mashariki ya Aleppo. Serikali imetuma wanajeshi 20,000 kuikomboa Aleppo dhidi ya waasi wasiozidi 8,000 wanaoushikilia mji huo wa kaskazini.

Uturuki yaionya Iran

Katika upande mwengine wa mgogoro wa Syria, Uturuki imeionya Iran dhidi ya lawama za Iran kwamba Uturuki inahusika na ghasia nchini Syria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, amesema hivi leo kwamba alimwambia mwenzake wa Iran, Ali Akbar Salehi, kwamba kauli ya hivi karibuni ya jenerali wa ngazi za juu wa jeshi la Iran, kwamba Uturuki inatekeleza mpango wa Marekani kuanzisha vita nchini Syria, haiwezi kustahmilika.

Watu wakitafuta miili iliyofukiwa na vifusi kufuatia mashambulizi ya jeshi la anga la Syria mjini Aleppo.
Watu wakitafuta miili iliyofukiwa na vifusi kufuatia mashambulizi ya jeshi la anga la Syria mjini Aleppo.Picha: Reuters

Davotuglu amesema kwamba alimwambia Salehi kwamba kauli hiyo ya Jenerali Hassan Firouzabadi haisaidii Iran wala Uturuki na kwamba, licha ya kuwa haikutolewa na viongozi wa kisiasa, bado ni wajibu wa maafisa wanaozifanyia kazi serikali zao kuwajibika kwa kauli zao.

Salehi alikwenda Uturuki kujaribu kurekebisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili, unaoonekana kuathiriwa na mgogoro wa Syria. Pia alikwenda kuomba msaada wa Uturuki katika kuachiwa kwa raia 48 wa Iran wanaoshikiliwa mateka na waasi nchini Syria, ambapo Davutoglu ameahidi kujaribu kusaidia.

Salehi ametangaza pia kufanyika kwa mkutano kuhusu Syria hapo kesho mjini Tehran, na kwamba mkutano huo utahudhuriwa na mataifa 13 kutoka Asia, Afrik a na Amerika ya Kusini, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran, IRNA. Hata hivyo, taarifa hiyo haitaji mataifa yatakayohudhuria mkutano huo, ambao Salehi anasema unalenga kumaliza ghasia na kuitisha mdahalo wa kitaifa nchini Syria.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Othman Miraji