1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaomboleza mauaji ya uwanja wa ndege

29 Juni 2016

Uturuki Jumatano (29.06.2016) imetangaza kuwa ni siku ya maombolezo ya taifa kufuatia shambulio la kigaidi katika uwanja wa ndege wa Istanbul hapo Jumanne lililouwa watu 41 wakiwemo wageni 13.

https://p.dw.com/p/1JFr4
Picha: Reuters/O. Orsal

Serikali ya Uturuki imeamuru bendera kupepea nusu mlingoti.Hapo mwaka jana serikali ilitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya miripuko miwili ya kujitolea muhanga kuuwa zaidi ya watu 100 katika mji mkuu wa Uturuki Ankara hapo mwezi wa Oktoba shambulio ambalo pia linadaiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu.

Uwanja wa ndege huo wa Atartak mojawapo ya uwanja wa ndege mkubwa kabisa katika kanda ulifungwa kwa msaa kadhaa baada ya shambulio hilo la kinyama. Ndege zilianza tena kutuwa kabla ya alfajiri leo hii na ndege za kwanza zilianza kuondoka asubuhi wakati uwanja wa ndege huo ukianza shughuli zake kwa kiasi fulani.

Ali Batur aliyempoteza kaka yake katika shambulio hilo amesema "Tufikirie nini ?Hatuwezi kufikiria chochote.Shambulio la kigaidi linaweza kutokea popote pale huwa linatokea kila mahala.Tatizo la ugaidi pia lipo katika nchi yetu.Mungu akijaalia haya tutayamaliza kwa kuwa na umoja na mshikamano."

Ushirikiano wa kimataifa dhidi ya ugaidi

Umoja wa kitaifa na ushirikiano wa dunia ndio wito ulitolewa na Waziri Mkuu wa Uturuki Benali Yidrim katika kupambana na ugaidi.

Hali baada ya shambulio la kigaidi katika uwanja wa ndege wa Istanbul.
Hali baada ya shambulio la kigaidi katika uwanja wa ndege wa Istanbul.Picha: picture-alliance/dpa/S. Suna

Amesema shambulio hilo kwa mara nyengine limeonyesha kwamba ugaidi ni tatizo la dunia na kudokeza kwamba linahusiana na kile alichokisema mafanikio ya Uturuki dhidi waasi wa Kikurdi halikadhalika hatua ilizochukuwa nchi hiyo hapo Jumatatu kurekebisha uhusiano wake na Israel na Urusi.

Wakati Yildrim akisema uchunguzi unaashiria kuhusika kwa kundi la Dola la Kiislamu katika shambulio hilo hakuna ishara kwamba kuna washambuliaji wengine waliofanikiwa kukimbia.Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo

Marekani ilitowa onyo la vitisho kwa Uturuki

Hapo Jumatatu wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitowa oyno la kuongezeka vitisho dhidi ya Uturuki nchi mwanachama mwenzake katika Jumuiya Kujihami ya NATO. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amelilaani shambulio hilo la uwanja wa ndege wa Istanbul.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Istanbul.
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Istanbul.Picha: Reuters/M. Sezer

Kerry amesema "Bado tunaendelea kukusanya taarifa na kujaribu kuyakinisha kile kilichotokea na nani aliefanya hayo na hatutoweza kuzunngumzia zaidi juu ya jambo hilo isipokuwa tu kwa kusema changamoto ya kwanza inyotubidi kukabiliane nayo ni kupambana na makundi ya kigaidi yanoyojihusisha na matumizi ya nguvu."

Mwaka jana uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul ni uwanja ulioshika nafasi ya 11 kwa kuwa na harakati nyingi sana duniani kwa kuwahudumia abiria milioni 61.8

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri :Yusuf Saumu